ARSENAL watakuwa leo wenyeji wa Aston Villa katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) linalotarajiwa kuwapa miamba hao jukwaa maridhawa la kulipiza kisasi dhidi ya kikosi hicho cha kocha Unai Emery. Itakuwa mara ya pili chini ya kipindi cha wiki nne kwa wagombezi hao halisi wa taji la EPL msimu huu kukutana, Villa wakipokeza Arsenal kichapo cha 2-1 mnamo Desemba 6 mjini Birmingham. Kwingineko, Manchester United wataalika Wolves uwanjani Old Trafford, Chelsea wakwaruzane na Bournemouth ugani Stamford Bridge nao Newcastle United wawaendee Burnley ugani Turf Moor. Brighton watakuwa wageni wa West Ham United huku Nottingham Forest wakialika Everton. Sawa na Villa waliopepeta Chelsea 2-1 ugani Stamford Bridge mnamo Jumamosi, masogora wa kocha Mikel Arteta nao walivuna ushindi sawa na huo dhidi ya Brighton katika EPL uwanjani Emirates, wikendi. Matokeo hayo yalidumisha Arsenal kileleni mwa jedwali kwa alama 42, tatu mbele ya Villa wanaokamata nafasi ya tatu. Miamba Manchester City wanashikilia nafasi ya pili kwa pointi 40 na kujikwaa kwa Arsenal kutawapa nafuu tele. Mechi dhidi ya Brighton ilikuwa ya tano mfululizo kwa Arsenal kushinda tangu Villa wawapokeze kichapo kichungu cha dakika za mwisho katika EPL uwanjani Villa Park. Aidha, wameshinda mechi tisa kati ya 10 zilizopita katika EPL ugani Emirates, zikiwemo sita za hivi karibuni. Matokeo hayo ni msururu wa mafanikio yao makubwa zaidi katika uwanja wao wa nyumbani tangu 2022. Ushindi mwingine hii leo utashuhudia wakifunga mwaka wa 2025 wakidhibiti kilele cha jedwali la EPL na hivyo kuweka hai matumaini ya kutwaa taji la kipute hicho kwa mara ya kwanza tangu 2003-04. Ingawa hivyo, kibarua kinachosubiri Arsenal si chepesi ikizingatiwa kwamba wamepoteza mechi tatu kati ya tano zilizopita dhidi ya Villa huku wakiokota alama nne pekee kutokana na michuano hiyo. Tofauti na Villa hata hivyo ambao wameshinda mechi mbili pekee kati ya 13 zilizopita za kufunga mwaka ligini, Arsenal wametamalaki kila mojawapo ya mechi za sampuli hiyo katika kipindi cha misimu minne kati ya mitano iliyopita. Motisha zaidi kwa Villa ni rekodi nzuri wanayojivunia ugani Emirates ikizingatiwa kwamba wametia kibindoni alama nne kutokana na mechi mbili zilizopita dhidi ya Arsenal ugenini. Waliwapokeza kichapo cha 2-0 mnamo Aprili 2024 kabla ya kuwalazimishia sare ya 2-2 mwanzoni mwa mwaka huu. Ushindi kwa kocha Emery, anayerejea Emirates alikowahi kuhudumu akinoa Arsenal, utashuhudia vijana wake wakifikia idadi ya alama zinazojivuniwa na waajiri wake hao wa zamani na hivyo kupandisha zaidi joto la EPL. Ikizingatiwa ugumu wa ratiba yao, Arsenal wanatarajiwa kufanyia kikosi chao mabadiliko makubwa baada ya majeraha kuwaweka nje mabeki Jurrien Timber, Riccardo Calafiori, Cristhian Mosquera na Ben White dhidi ya Brighton.