RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amejitokeza wazi kukanusha madai kuwa anahusika katika mipango ya kuvuruga au kudhoofisha Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), akisema hana nia wala sababu ya kuingilia masuala ya ndani ya chama hicho. Uhuru alitoa kauli hiyo wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Lugari, marehemu Cyrus Jirongo, yaliyofanyika Lumakanda, Kaunti ya Kakamega. Akizungumza mbele ya viongozi wa kitaifa na maelfu ya waombolezaji, Uhuru alisema kumekuwa na juhudi za kumhusisha na njama za kisiasa zinazolenga kuvuruga vyama vya siasa, hususan ODM, jambo alilolisema halina msingi wowote. “Mimi ni mstaafu. Sina haja ya kuvuruga ODM wala chama chochote. Kila chama kina wamiliki wake na njia zake za kushughulikia masuala yake,” alisema Uhuru, kauli iliyochukuliwa kama ujumbe wa moja kwa moja kwa Rais William Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza. Uhuru alisisitiza kuwa anachotetea ni kuwepo kwa demokrasia imara ya vyama vingi, ambapo kila chama kinaheshimiwa na kuachiwa nafasi ya kufanya maamuzi bila shinikizo au hila za kisiasa. “Tunachotaka ni demokrasia hai. Vyama vijengwe, si kuvunjwa. Ukishindwa kushawishi watu wajiunge na wewe, usitafute wa kulaumu,” aliongeza. Kauli hiyo ilijiri huku kukiwa na madai ya mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya viongozi wa ODM na Kenya Kwanza kwamba kuna njama za nje za kukidhoofisha chama hicho au kukivuruga kutoka ndani. Uhuru alisema madai hayo ni kisingizio cha kushindwa kwa wengine kujenga maridhiano ya kisiasa kwa hiari. “Mtu akishindwa njia ya kujipendekeza kule anataka kujipendekeza, lazima atafute mtu aseme kuwa watu wanakataa kukusikiza kwa sababu ya yule na huyu.” Akimrejelea marehemu Cyrus Jirongo, Uhuru alisema kiongozi huyo alikuwa mfano wa mwanasiasa aliyethamini sana uhuru wa vyama na mazungumzo ya kisiasa, akifanya kazi na pande zote bila kuvunja misingi ya demokrasia. “Cyrus Jirongo aliamini katika heshima ya vyama vya siasa na alifanya kazi kuvuka mipaka ya vyama bila kuua au kumeza vingine. Huo ndio urithi tunaopaswa kuendeleza,” alisema. Uhuru aliwataka viongozi wanaoendeleza migawanyiko ndani ya ODM kuacha kile alichokitaja kuwa ni “fikira mbovu”, na badala yake waende kwa wananchi, wajenge chama chao cha kisiasa, waweke wazi sera zao na wazisimamie kwa ujasiri. “Toa hiyo fikira mbovu, enda zungumza na wananchi. Unda na usimamishe chama chako. Kuwa na sera zako kama mwanaume,” alisema Uhuru. Uhuru pia aliwakosoa vikali viongozi ambao, kwa mtazamo wake, huzunguka katika ulingo wa kisiasa wakitoa kauli za uchochezi zisizo na mchango wowote wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa wala kukuza demokrasia. “Sio kuzunguka huku na kule ukitoa mambo ya upuzi ambayo haipeleki nchi mbali,” alisema. Akisisitiza maono yake kwa taifa hata baada ya kustaafu, Uhuru aliwakumbusha Wakenya umuhimu wa kudumisha umoja wa kitaifa, demokrasia na kuheshimu uamuzi wa wananchi. “Tunataka nchi iliyo na umoja, tunataka demokrasia, na tunataka matakwa ya wananchi yaheshimiwe,” aliongeza. Huku akikumbusha wakosoaji wake kuwa sasa ni kiongozi mstaafu, Uhuru aliweka wazi kuwa kustaafu hakumaanishi udhaifu wala kukubali kudharauliwa. “Sitaki kusema mengi kwa sababu mimi ni mstaafu, lakini kwa kusema mstaafu sisemi uniingize kidole kwa macho; mimi pia nitakuingiza. Tuheshimiane,” alionya. Kauli za Uhuru zilijiri wakati ambapo mvutano unaendelea kushuhudiwa ndani ya ODM, ambapo baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho wamemlaumu hadharani kwa madai ya kuingilia masuala ya ndani ya chama na kuchochea migawanyiko. Uongozi wa juu wa ODM, ukiongozwa na mwenyekiti wake Gavana Gladys Wanga pamoja na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, umemshutumu Uhuru kwa madai ya kupanga kutumia wanachama wa ndani ya chama hicho kusababisha migawanyiko ya kisiasa katika ODM.