Cheche kali za siasa mazishi ya Jirongo lawama mpya zikizuka kuhusu alivyoangamia

MAZISHI ya aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo yaligeuzwa kuwa jukwaa la siasa kali, lawama na maswali mazito kuhusu mazingira ya kifo chake, huku viongozi wa kisiasa wakitaka uchunguzi wa kina wa kitaalamu kuhusu ajali iliyomuua. Akizungumza wakati wa mazishi hayo yaliyofanyika Lumakanda, Kaunti ya Kakamega jana, aliyekuwa Seneta wa Vihiga George Khaniri alirusha kombora la kisiasa alipodai kuwa wachunguzi wa kibinafsi wamepata ushahidi unaozua maswali mapya kuhusu ajali hiyo. “Kuna wachunguzi wa kibinafsi ambao wamekuwa wakifuatilia haya maneno. Wamepata picha za CCTV na wanafanya uchambuzi,” Khaniri aliwaambia waombolezaji. Alidai kuwa kamera za CCTV katika kituo cha mafuta cha Naivasha zilionyesha kuwa gari la Jirongo lilikuwa na abiria mwingine kwenye kiti cha mbele muda mfupi kabla ya ajali. “Ukiangalia lile gari lilipoingia kwa kituo cha mafuta huko Naivasha, halikuwa na mtu mmoja. Kulikuwa na mtu ameketi pale mbele,” alidai Khaniri. Kauli hiyo ilizua kimya kizito kabla ya kelele za mshangao kutoka kwa umati. Khaniri alihoji kwa nini Jirongo alipatikana peke yake baada ya ajali. “Sasa likitoka hapo (gari) likapata ajali, huyo mtu mwingine ako wapi? Mbona Jirongo alipatikana peke yake kwenye gari? Kuna mapengo mengi sana. Tunataka uchunguzi wa kina wa kitaalamu,” alisema. Mbunge wa Saboti Caleb Amisi naye alitumia lugha kali, akilaumu serikali kwa kile alichoita ukimya wa kushangaza. Amisi alielekeza lawama kwa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliyehudhuria akimtaka aende kwa Rais William Ruto kumshinikiza aagize uchunguzi kuhusu kifo cha Jirongo. Alikumbusha hadithi ya zamani ambapo Jirongo alimkabili aliyekuwa Rais Daniel arap Moi ili kulinda wadhifa wa Mudavadi serikalini. “Cyrus alienda kwa Moi bila kuogopa akasema Musalia asifukuzwe. Sasa historia inakurudia. Rafiki ni yule anakutambua kwa shida,” Amisi aliongeza, huku umati ukishangilia. Maswali kuhusu ajali hiyo yalianza hata kabla ya mazishi. Aliyekuwa Mbunge wa Westlands Fred Gumo alisema ni jambo la kushangaza kwamba, hakuna hata abiria mmoja kutoka kwa basi lililohusishwa na ajali hiyo aliyejitokeza kueleza kilichotokea. “Wananchi wanauliza maswali mengi. Haiaminiki,” Gumo alisema alipokuwa akizungumza katika ibada ya kumbukumbu nyumbani kwa Jirongo mjini Kitale. Alisema basi hilo lilikuwa likielekea Busia na huenda lilikuwa limebeba abiria wengi kutoka Magharibi mwa Kenya. “Na hakuna hata mtu mmoja amejitokeza kusema alikuwa kwa basi lilihusika kwenye ajali Naivasha? Watu walitembea wakaenda? Wapi?” alihoji. Wakati huo huo, Gavana wa Siaya James Orengo alitumia mazishi hayo kutetea vikali Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna dhidi ya mashambulizi kutoka kwa wanachama wa chama hicho. “Mimi ninamtambua Sifuna kama Katibu Mkuu wa ODM. “Raila mwenyewe alisema msemaji wa chama ni Edwin Sifuna. Huo ndio ukweli kisheria,” alisema Orengo. Alionya dhidi ya juhudi za “kumezwa kwa vyama vya kisiasa” akisema hilo ni tishio kwa demokrasia. “Vyama vinamezwa moja moja. Rafiki yangu Musalia Mudavadi chama chake kilimezwa. Ford Kenya kinatafunwa, ODM pia. Hatuwezi kukubali. Demokrasia lazima ilindwe,” alisema. Seneta wa Kakamega Boni Khalwale naye alimgeukia Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, akimtaka aeleze hadharani mikutano yake ya mara kwa mara na Jirongo kabla ya kifo chake. Alidai kuwa alikuwa akimwona Jirongo mara kwa mara akiingia ofisi ya Spika Bungeni kwa dakika 30 hadi saa moja. “Kuna kitu katika uhalifu kinaitwa sababu. Jirongo ama alikufa kwa sababu ya siasa au biashara,” Khalwale aliongeza. Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha DAP- Kenya, alisema serikali imefeli kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kifo cha Jirongo. Bw Sifuna, alitumia mazishi hayo kuomba radhi Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye pia alihudhuria kufuatia mashambulizi ya kisiasa yanayoelekezwa kwake na baadhi ya vigogo wa chama hicho. Sifuna alisema ni makosa kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho kumshambulia Uhuru ilhali ndiye aliyesimama bega kwa bega na aliyekuwa kiongozi wa ODM, marehemu Raila Odinga, katika harakati za kuwania urais. Kauli hiyo ilipokelewa kwa shangwe na baadhi ya waombolezaji, huku ikidhihirisha mgawanyiko unaoendelea ndani ya ODM kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho baada ya kifo cha Raila Odinga.