MITANDAO ya kijamii imejaa mijadala inayozungumzia suala kuwa Wakenya wengi hawawezi kuchutama ipasavyo, hasa wale wanaolazimika kutumia vyoo vya mashimo vijijini wakati wa likizo ndefu ya Desemba. Kejeli zinasema baadhi yao wamelazimika kuahirisha haja kubwa hadi watakaporejea mijini, huku wengine wakichagua kwenda hotelini, si kula, bali kutumia vyoo vya kisasa. Hata hivyo, wataalamu wa magonjwa ya mfumo mmeng’enyo wa chakula wanasema mtu anafaa kutumia choo cha shimo kwa sababu kuchutama ndiko kunasaidia haja kubwa kutoka ipasavyo na utumbo mkubwa kusafishwa kikamilifu. Dkt Amos Mwasamwaja, daktari wa mfumo wa mmeng’enyo chakula katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, anaeleza kwa nini kuchutama kunafaa kuwa mkao wakati wa haja kubwa. “Kunapunguza muda unaotumia chooni, na hurahisisha kutoka kwa haja kubwa. Kunasaidia haja kubwa kusonga, tofauti na kukaa.” Anasema kukaa kwenye vyoo vya kisasa kunaongeza kujikaza wakati wa haja kubwa. “Hili si tu hupunguza kasi ya kutoka kwahaja kubwa na kumfanya mtu kukaa chooni kwa muda mrefu, bali pia huleta hisia ya kutomaliza haja kikamilifu,” anaeleza. “Mtu anaweza kutoa haja kubwa lakini bado ahisi hajamaliza, jambo ambalo ni mojawapo ya tatizo la kufunga choo.” Akielezea kuhusu faida za kuchuchumaa, anaongeza: “Kuchutama kunaruhusu haja kubwa kupita bila upinzani mkubwa. Hii hupunguza kujikaza na muda wa kukaa chooni.” Dkt Mwasamwaja anasema kukaa badala ya kuchutama, kunaweza kuchangia hatari ya kufunga choo. “Ni hatari. Kujikaza huongeza shinikizo kwenye mishipa ya damu iliyo karibu na tundu la haja kubwa, na baada ya muda, hii inaweza kusababisha kuvimba au hata sehemu ya utumbo kutoka nje,” anasema. Kwa wale wasioweza kuchutama, anapendekeza kuinua miguu kwa kutumia kigoda kidogo. “Kuinua magoti juu ya nyonga hufungua njia ya choo. Kutumia kigoda ukiwa umekaa kwenye choo cha kisasa ni mbadala mzuri inayorahisisha kutoka kwa haja kubwa.” Utafiti wa kisayansi unaunga hoja hii. Utafiti wa mwaka 2010 uliochapishwa katika jarida la Low Urinary Tract Symptoms ulibaini kuwa kuchutama wakati wa haja kubwa hunyoosha njia ya choo na haja kubwa, na hivyo kurahisisha kutoka kwa haja kubwa. Utafiti wa awali wa mwaka 2003 uliochapishwa katika jarida la Digestive Diseases and Sciences pia ulithibitisha hilo. Utafiti huo uliwahusisha watu 28 wenye afya na kubaini kuwa kuchutama hupunguza kwa kiasi kikubwa muda unaohitajika kuhisi kuwa mtu amemaliza haja pamoja na juhudi za kujikaza, ikilinganishwa na kukaa kwenye choo cha kawaida au cha chini. Watafiti walihitimisha kuwa kukaa kunahitaji kujikaza kupita kiasi ikilinganishwa na kuchutama. Dkt Alemanji Ajua, daktari mwingine wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan na rais wa Chama cha Madaktari wa Mfumo wa Chakula nchini Kenya, anaongeza kuwa kwenda haja hutegemea uwiano wa kimaumbile, uratibu wa misuli na mwili. Dkt Ajua anaonya kuwa choo cha kukalia husababisha kujikaza kupita kiasi. Baada ya muda, hili linaweza kuchangia matatizo mengine ya eneo la haja kubwa, kama vile michubuko midogo inayosababisha kutokwa na damu. Kutomaliza haja kikamilifu pia kunaweza kusababisha gesi kujaa tumboni na maumivu ya tumbo.