WAKILI mmoja amewasilisha kesi mahakamani akitaka agizo la kupiga marufuku muziki wa sauti ya juu katika magari ya uchukuzi wa umma (PSV), akisema kuwa tabia hiyo inakiuka haki kadhaa za kikatiba za wasafiri na ni sawa na mateso ya kisaikolojia. Bw Samuel Borongo Nyamari anasema katika kesi yake kuwa ameishi Nairobi kwa kipindi cha miaka sita iliyopita na amekuwa akitegemea usafiri wa umma, maarufu kama matatu, kila siku. Hata hivyo, anasema katika kipindi hicho, yeye na wasafiri wengine wamekuwa wakikumbwa na kile anachokitaja kama uchafuzi wa utulivu usiokoma unaotokana na muziki wa sauti ya juu, na unaorudiwa mara kwa mara unaochezwa ndani ya magari ya uchukuzi wa umma. “Ni jambo linalojulikana wazi na linaloweza kutambuliwa kirahisi na mahakama kuwa idadi kubwa mno ya matatu jijini Nairobi yana mifumo mikubwa ya muziki na hupiga muziki siku nzima kwa abiria wao,” alisema katika kesi yake. Anasema kucheza muziki wa sauti ya juu unaosababisha uchafuzi wa kelele kwenye matatu kunakiuka haki yake ya msingi ya kuwa na mazingira safi na yenye afya chini ya Kifungu cha 42 cha Katiba. Bw Nyamari anasema wahudumu wa matatu hawazingatii watoto wachanga na wenye masikio dhaifu, wazee, wagonjwa na watu wenye changamoto nyingine za hisia, au abiria wanaotaka kupiga au kupokea simu au kusafiri kwa amani. Mlalamishi huyo anaongeza kuwa kucheza muziki wa sauti ya juu wenye midundo mizito na usiokoma kwa watumiaji wa matatu ni aina ya vurugu dhidi ya abiria. Bw Nyamari pia anasema wahudumu wa matatu hushindwa kuwaarifu na kuwaonya Wakenya kuhusu muziki wa sauti ya juu kabla ya kupanda magari hayo, na badala yake huwavamia wasafiri wasiotarajia kwa muziki mkali mara tu safari inapoanza. Anasisitiza kuwa muziki wa sauti ya juu ni sawa na mateso ya kisaikolojia na umeibua kile anachokitaja kama “janga la kimya kimya” linalowaathiri maelfu ya wasafiri kila siku. Katika kesi yake, mlalamishi anadai kuwa tabia hiyo inakiuka haki ya kikatiba ya kuwa na mazingira safi na yenye afya chini ya Kifungu cha 42, akisema kelele kupita kiasi ni aina ya uchafuzi wa mazingira. Pia anadai ukiukaji wa haki ya uhuru na usalama wa mtu binafsi chini ya Kifungu cha 29. Aidha, kesi hiyo inataja ukiukaji wa haki za watumiaji chini ya Kifungu cha 46 cha Katiba, ikisema kuwa abiria wananyimwa huduma zenye ubora unaofaa na hawapewi taarifa muhimu zinazowawezesha kufaidika kikamilifu na huduma za uchukuzi wa umma. Haki ya kupata kiwango cha juu zaidi cha afya kinachowezekana chini ya Kifungu cha 43 pia imetajwa, Nyamari akisema kuwa kukaa muda mrefu kwenye mazingira ya muziki wa sauti ya juu kunahatarisha afya ya jumla ya watoto, wazee na watu wenye hali nyingine za kiafya. Miongoni mwa maagizo anayoomba mahakamani, mlalamishi anataka itangazwe kuwa kuchezwa kwa muziki wa sauti ya juu katika magari ya uchukuzi wa umma ni kinyume cha Katiba na kunakiuka Vifungu vya 29, 42, 43 na 46 vya Katiba. Pia anataka amri itolewe kupiga marufuku magari yote ya uchukuzi wa umma kucheza muziki wa sauti ya juu. Ametaja Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA), Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) na Chama cha Wamiliki wa Matatu kama washtakiwa katika kesi hiyo.