2026: Mwaka wa maamuzi mazito na kujipanga kisawasawa

HATA kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kuchapishwa na kampeni kuanza rasmi, mwaka wa 2026 utakuwa muhimu kwa wanasiasa huku wakijiandaa. Wachambuzi wa siasa wanasema uchaguzi wa Agosti 2027 utategemea mikakati na maamuzi yatakayofanywa mwaka wa 2026. Ingawa Uchaguzi Mkuu ujao utatoa washindi na walioshindwa, ni mwaka wa 2026 utakaoimarisha miungano ya kisiasa, mageuzi ya taasisi, mienendo ya wapigakura na hali ya uchumi itakayoamua mwelekeo wa taifa. Kwa mtazamo mpana, wachambuzi wa siasa wanaamini 2026 ndio mwaka ambao maswali ambayo hayajapatiwa majibu nchini yatabainika. Je, ahadi za 2022 zitatimizwa au zitasambaratika kutokana na uchovu wa umma; je, tabaka la wanasiasa litabadilika na kukabiliana na wapigakura wasioridhika? “Ni mwaka ambao miungano itakuwa migumu, wapigakura watajipanga upya, marekebisho ya Katiba yatapitishwa au yatakwama, na taasisi kama Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zitajaribiwa kabla ya kura yoyote kupigwa,” anasema mchambuzi wa siasa Dismas Mokua. Anaongeza: “Uchaguzi mkuu ujao unaweza kuwa 2027, lakini watakaoshinda au kushindwa wataamuliwa 2026, mwaka unaotarajiwa kubainisha miungano, mageuzi na mipaka ya uvumilivu wa wananchi.” Mwaka huu wa 2026, minong’ono ya siasa itabadilika na kuwa maamuzi magumu, huku miungano ya kabla ya uchaguzi ikirasmishwa na mgombea urais wa upinzani akiteuliwa kumpinga Rais William Ruto. Miongoni mwa hatua zenye uzito mkubwa ni chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais Ruto kuungana rasmi na Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kilichoanzishwa na marehemu Raila Odinga. Kwa mujibu wa wandani wa vyama hivyo, vinapanga kutia saini makubaliano rasmi ya muungano kabla ya uchaguzi wa 2027, hatua itakayofanya ODM kuunga mkono azma ya Rais Ruto kuchaguliwa tena. Kwa Rais Ruto, muungano huo utakuwa kilele cha mkakati wake baada ya maandamano ya Gen Z alipounda serikali jumuishi na kuigeuza kuwa chombo thabiti cha uchaguzi. Kwa ODM, utaashiria mabadiliko ya kihistoria baada ya kifo cha kiongozi wake ambaye alitawala siasa za upinzani kwa zaidi ya miongo mitatu. Lakini huku upande wa serikali ukiimarisha misingi yake, upinzani unakabiliwa na shinikizo la kusuluhisha masuala yake ya ndani. Muungano wa Upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa DCP na Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic Front, umeweka mwisho wa Machi 2026 kutaja mgombea urais wake. Katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka 2025, Bw Musyoka alitangaza kuwa muungano huo utamtangaza mgombea wake wa urais kufikia Machi 2026, akisema hatua hiyo itaonyesha umoja na kwamba wako tayari kupambana na kile alichoita “utawala dhalimu na uliokosa mwelekeo kimaadili”. Hata hivyo, tishio kubwa kwa upinzani mwaka wa 2026 si ukosefu wa mgombea urais, bali kushindwa kuafikiana mapema kuhusu mmoja wao atakayesuka muungano wa kitaifa wenye uwezo wa kushindana na Rais Ruto. Mwaka wa 2026 pia utakuwa mwaka ambao makundi makuu ya wapigakura yatahamia pande tofauti au kujikita zaidi wanakounga mkono. Wachambuzi wanasema mkakati wa Rais Ruto unategemea nguzo tatu: kupanua muungano, kugawanya upinzani, na kupangua hesabu za kikanda. Mtaalamu wa siasa Martin Oloo anasema Rais Ruto anafahamu kufifia kwa uungwaji mkono wake katika Mlima Kenya, na hivyo ameamua kukumbatia Nyanza, Magharibi na Pwani ili kuimarisha ngome zake. Kifo cha Raila Odinga, hata hivyo, kimeleta sintofahamu mpya kuelekea 2026 na kuendelea. Naibu kiongozi wa Safina, Willis Otieno, anataja kifo hicho kuwa “tukio la kipekee” litakalobadilisha sura ya siasa za Kenya kwa miaka mingi. Wakati huo huo, Mlima Kenya linasalia kuwa eneo tete. Wachambuzi wanasema Bw Gachagua anajisawiri kama msemaji wa kisiasa wa eneo hilo, mkakati unaoweza kubadilisha siasa. Miongoni mwa masuala yatakayojaribu siasa Kenya 2026 ni msukumo wa marekebisho ya Katiba. Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amependekeza mabadiliko makubwa yatakayobadilisha mamlaka kati ya Serikali Kuu, Bunge na Kaunti. Iwapo ajenda ya kura ya maamuzi itaendelea au itakwama 2026, itaathiri pakubwa miungano, wapigakura na uaminifu wa siasa kuelekea 2027. Jaribio jingine muhimu lakini tulivu mwaka wa 2026 litakuwa kuhusu iwapo IEBC imejiandaa kwa uchaguzi. Mwenyekiti wa tume hiyo, Erastus Ethekon, amesema IEBC iko tayari, ikipanga kusajili wapigakura wapya 6.3 milioni, asilimia 70 wao wakiwa vijana. Kufikia wakati Wakenya watakapopiga kura 2027, maamuzi mengi muhimu yatakuwa tayari yamefanywa kimyakimya kwenye vyumba vya mikutano 2026, kwa sauti kwenye mikutano ya hadhara, na polepole kupitia taasisi zinazokabiliwa na shinikizo.