Mwaka Mpya 2026: Ahadi za Ruto alizotoa 2022 zaingia kipindi cha lala salama

RAIS William Ruto anakabiliwa na mwaka mgumu 2026 huku akibadili mkondo kuelekea awamu ya mwisho ya kutekeleza ahadi zake za kiuchumi, akishuhudia mafanikio na misukosuko kutokana na uhaba wa rasilmali za kutimiza ahadi nyingi ambazo hazijatekelezwa. Kwa ujumla, uchumi unatarajiwa kuimarika mwaka mpya huku biashara zikionyesha matumaini kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa mahitaji, hali inayoweza kuchochea uundaji wa ajira, kufuatia kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa na viwango vya riba. Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 9.6 Oktoba 2022 hadi asilimia 4.5 mwezi uliopita, hali iliyopunguza shinikizo kwa watumiaji waliokumbwa na gharama ya juu ya maisha tangu janga la Covid-19 mnamo 2020. Benki Kuu ya Kenya (CBK) pia imepunguza kiwango cha riba ya msingi mara nane tangu mwaka jana, kutoka asilimia 13 hadi asilimia 9.25 kufikia Oktoba 2025, hatua iliyochochea ongezeko la mikopo ya benki kwa biashara. Mwelekeo huu wa kiuchumi umeifanya Benki ya Dunia kurekebisha makadirio ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ya Kenya kwa 2025 kutoka asilimia 4.5 hadi 4.9. Hata hivyo, tathmini ya kina ya utekelezaji wa mipango aliyoahidi Rais inaonyesha kuwa baadhi inaendelea polepole huku mingine ikikosa kufikia malengo, jambo linalomletea changamoto kubwa anapojitayarisha kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao. Ahadi ya kuanzisha maeneo 47 ya viwanda katika kila Kaunti kufikia Juni 2025 haikutimia. Kaunti 10 pekee zilipata ufadhili kamili kufikia Juni, huku 24 zikitarajiwa kupata fedha katika mwaka wa sasa wa kifedha. Katika sekta ya makazi, serikali imekamilisha nyumba 8,367 kati ya Septemba 2022 na Desemba 13, 2025, ikilinganishwa na lengo la nyumba 200,000 kwa mwaka. Serikali inasema nyumba 234,910 ziko katika awamu tofauti za ujenzi, ikilenga kukamilisha nyumba 500,000 kufikia Juni 2029.