KIONGOZI wa chama cha Safina, Jimi Wanjigi, amewataka viongozi wa upinzani kuachana na kile alichokitaja kuwa “siasa wa kizazi cha zamani” na badala yake wajenge umoja unaojikita katika kutatua matatizo halisi yanayowakumba Wakenya wa kawaida. Bw Wanjigi, ambaye pia ametangaza nia ya kugombea urais, alisema kumuondoa Rais William Ruto mamlakani hakuwezi kuwa msingi pekee wa kuunganisha upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. “Tunaongea sana kuhusu kuungana ili kumshinda Ruto. Huo si msingi,” alisema, akionya kuwa muungano wowote usiogusia malalamishi ya kiuchumi yaliyosababisha maandamano ya wananchi hautadumu. Katika mahojiano maalum na Taifa Leo , Bw Wanjigi alisema Wakenya wanataka suluhu kuhusu ukosefu wa ajira, mzigo wa ushuru na gharama ya juu ya maisha, lakini viongozi wa kisiasa wamekwama katika siasa za majabiliano badala ya kusikiliza wananchi. Alitabiri kuwa kinyang’anyiro cha urais 2027 kitabainishwa na ajenda za kiuchumi, si ukabila au maeneo. Alipuuza juhudi za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua za kuunda Muungano wa upinzani, akizitaja kama “muungano wa kieneo” usioweza kufanikiwa. “Gachagua amechagua njia ya kikabila. Hizo si siasa za Safina,” alisema. “Tunaamini umoja wetu unatokana na maumivu ya pamoja ya kiuchumi, si hesabu za kikabila.” Bw Wanjigi alisema uchaguzi ujao unapaswa kuleta “uhuru wa tatu” katika mapinduzi ya mawazo, na wala si bunduki wala kauli mbiu. Alisema maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2024 yalikuwa kura ya maoni ya katikati ya muhula dhidi ya utawala mbovu wa Rais Ruto. "Hayo yalikuwa mapinduzi ya kizalendo yaliyoongozwa na vijana,” alisema. “Ruto alipoteza uhalali wake wakati huo.” Kuhusu ODM kushirikiana na Rais Ruto, Bw Wanjigi alisema hawezi kuunga mkono. “Lakini ODM ikijitenga na Ruto, tunaweza kuzungumza,” alisema. Aliongeza kuwa Safina inalenga kuimarisha uwajibikaji wa polisi kwa wananchi na kujenga mtandao wa kitaifa unaojikita katika hoja na si ukabila. “Huu si wakati wa siasa za kale,” alisema. “Uhuru ujao ni wa kiuchumi, na unaanza sasa.”