Tanzania yaangukia kismati cha 16-bora AFCON baada ya miaka 45

TANZANIA imepenya awamu ya 16-bora ya Kombe la Afrika (AFCON) 2025 kwa bahati ya mtende pasipo kushinda mechi yoyote, baada ya kuagana sare ya 1-1 na Tunisia katika uwanja wa Rabat Olympic nchini Morocco, Jumanne usiku. Sare hiyo ilitosha kuzipa timu hizo tikiti ya 16-bora. Tunisia, ambao ni mabingwa wa makala ya 2004, walihitaji alama moja pekee kunata katika nafasi ya pili kundini nyuma ya vinara Nigeria. Lakini matokeo hayo yalifaidi zaidi Taifa Stars ya Tanzania ambayo imekuwa nchi ya kwanza kutua 16-bora ya AFCON na alama mbili pekee tangu dimba hilo liongezwe idadi ya timu hadi 24 mnamo 2019. Vile vile, Tanzania, ambayo inashiriki AFCON kwa mara ya nne, imefuzu awamu hiyo ya muondoano kwa mara yake ya kwanza kabisa tangu waanze kushiriki mwaka wa 1980. Wawakilishi hao wa kanda ya Afrika Mashariki walipenya kwa kuwa timu ya nne bora zaidi kati ya sita zilizomaliza kwenye nafasi ya tatu makundini. Walipiku Angola kwa idadi ya magoli waliyofunga (3 ikilinganishwa na 2) kwani timu zote zilikuwa na alama mbili. Mnamo Jumanne usiku, Ismael Gharbi aliwapa Tunisia uongozi kupitia penalti dakika ya 43. Lakini Feisal Salum alisawazisha 1-1 mapema kipindi cha pili kuweka hai matumaini ya Tanzania kupenyeza hadi 16-bora, na kwa bahati mechi ikakamilika kwa sare hiyo kuhakikisha Taifa Stars wanaweka historia. Tanzania walikuwa wamepoteza mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Nigeria kabla kutoka sare na majirani wao wa Afrika Mashariki, Uganda. Hivyo sare na Tunisia ilitosha kwao kupata nyota ya jaha na sasa wamefuzu kwa michuano ya 16-bora kwa mara ya kwanza kabisa katika miaka 45. Katika mechi nyingine ya Jumanne usiku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) walilima Botswana 3-0 kumaliza katika nafasi ya pili Kundi D nyuma ya Senegal. Wavuta-mkia Botswana tayari walikuwa wamebanduliwa AFCON na wanaondoka na alama sufuri. DR Congo walikuwa wamehakikishiwa tikiti ya 16-bora kabla mechi hiyo uwanjani Al Medina mjini Rabat. Nao vinara Senegal walihakikisha wanamaliza kidedea juu ya kundi loa kwa kupepeta Benin 3-0 katika uwanja wa Tangier Grand Stadium mjini Tangier. Hii ni licha ya Senegal kusalia wachezaji 10 baada ya Kalidou Koulibaly kulishwa kadi nyekundu dakika ya 71. Senegal walipiku DR Congo kileleni mwa kundi kutokana na ubora wa magoli kwani timu hizo zilikuwa na alama saba kila moja. Nao Super Eagles wa Nigeria walitonesha kidonda cha Uganda Cranes kwa kuwahemesha 3-1. Uganda, ambao tayari walikuwa wameshabanduliwa dimbani, waliona usiku mrefu huku wakilazimika kubadilisha golikipia mara mbili kutokana na jeraha kisha kadi nyekundu iliyowaacha wachezaji 10. Nathanael Mukau alifungua ukurasa wa magoli dakika ya 31. Gael Kakuta akatinga la pili kupitia penalti dakika ya 41, kabla kufunga kazi kwa bao lake la pili na la tatu la timu dakika ya 60. Abdoulaye Seck alifungua ukurasa wa magoli dakika ya 38, Habib Diallo akatumbukiza wavuni pasi safi ya nyota Sadio Mane dakika ya 62 kabla Cherif Ndiaye kusukuma kombora la penalti dakika ya 97 na kuondoa wasiwasi wa kadi ya Koulibaly.