ODM ikiamua kugombea urais mjue mimi ndiye nitabeba bendera, Oburu awaka

KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, amesema atakuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 iwapo ODM itaamua kuwania uchaguzi huo kivyake. Akizungumza akiwa Diani, Kaunti ya Kwale, alipokuwa akitoa ujumbe wake wa Mwaka Mpya kwa Wakenya na wafuasi wa ODM, Dkt Oburu Oginga alisema mwaka wa 2026 utakuwa muhimu kwa chama hicho kuamua mwelekeo wake wa kisiasa. Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa katiba ya ODM, kiongozi wa chama ndiye mgombea wa urais moja kwa moja, jambo linalomaanisha kuwa atakabiliana na Rais William Ruto mwaka ujao iwapo chama kitaamua kushiriki uchaguzi bila kushirikiana na vyama vingine. “Na bila shaka, iwapo tutaamua kwenda pekee yetu, nataka iwe wazi kabisa kwamba katiba ya chama chetu tayari ina mgombeaji wa urais. Na mgombeaji huyo wa urais ametajwa wazi katika katiba ya chama. Naye ni kiongozi wa chama. Mimi ndiye mgombeaji wa urais wa ODM endapo ODM itaamua kwenda kivyake,” alisema Dkt Oginga. Kiongozi huyo wa ODM pia alionya kuwa, mwanachama yeyote wa chama mwenye ndoto ya kuwania urais anapaswa kutafuta chama kingine cha kisiasa. Alieleza kuwa kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2026, chama kitakuwa kimeamua iwapo kitashiriki kivyake au kitaungana na vyama vingine, na kufikia wakati huo, ODM pia itakuwa imejua washirika itakaoungana nao endapo itaunda muungano. Dkt Oginga alibainisha kuwa, kwa sasa ODM bado iko katika ushirikiano na serikali ya Kenya Kwanza, lakini akasisitiza kuwa chama hicho hakijajiunga kikamilifu serikalini na kinaendelea kuimarisha miundo yake huku kikidumisha uhuru wake, ingawa kimeacha wazi uwezekano wa kuungana na Rais Ruto kulingana na maamuzi yatakayofanywa kabla ya uchaguzi wa 2027. “Kufikia mwisho wa 2026, chama chetu kitakuwa kimejua iwapo tutashiriki (uchaguzi mkuu wa 2027) kivyetu au tutaungana na vyama vingine,” alisema kiongozi huyo wa chama. Akiwatakia Wakenya Mwaka Mpya mwema na wenye mafanikio, Dkt Oginga alikumbuka kwa huzuni kifo cha ndugu yake, aliyekuwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, pamoja na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu utekelezaji kamili wa ajenda ya vipengele 10 kati ya ODM na serikali ya Kenya Kwanza. “Tunaangalia kwa makini utekelezaji wa ajenda hizo za makubaliano tuliyofanya nao. Kuhusu kama tutafanikiwa katika utekelezaji wake, ni Mungu pekee anayejua,” alisema kiongozi huyo wa chama. Alisisitiza kuwa licha ya changamoto hizo, ODM bado ni chama imara chenye mizizi imara mashinani, na kinaendelea kujipanga upya na kuimarisha miundo yake kuelekea uchaguzi wa 2027. Pia, aliwahimiza wanachama kubaki makini na kujitolea kwa maslahi ya wananchi kama ilivyoelezwa katika malengo ya chama, akisema uthabiti wa ODM utakuwa muhimu katika mwaka huu muhimu kabla ya uchaguzi mkuu. Seneta huyo wa Siaya pia alisisitiza kuwa ODM haiuzwi, akikanusha madai yanayodokeza hivyo. “Chama hiki hakiuzwi, hakitawahi kuuzwa, ni kikubwa mno kuuzwa kwa yeyote,” alisema, akisisitiza umaarufu wa chama hicho mashinani na uhuru wake.