RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amewasifu vijana wa Afrika akiwataja kuwa rasilmali kubwa zaidi ya bara lao, na kuwataka wajitokeze kwa ujasiri, uadilifu na maono, akisisitiza kuwa mabadiliko ya Afrika yatachochewa na Waafrika wenyewe wala si suluhu kutoka nje. Akizungumza Jumatano jioni wakati wa hafla ya Future Africa Leaders Awards (FALA) 2025 iliyofanyika katika uwanja wa Loveworld Nation Arena jijini Lagos, Nigeria, ambako alikuwa mgeni wa heshima kwa mwaliko wa Mchungaji Chris Oyakhilome, Bw Kenyatta alisema utajiri wa kweli wa Afrika haupo chini ya ardhi bali unapatikana katika fikra na mioyo ya watu wake. “Tumeambiwa mara nyingi kuhusu utajiri mkubwa ulio chini ya ardhi ya Afrika, lakini rasilmali yetu kuu iko katika akili na mioyo ya vijana wetu. Ninyi si viongozi wa kesho; ninyi ni viongozi wa leo mnaoamua kesho,” alisema. Aliwasifu washindi wa tuzo hizo kwa huduma na ubunifu wao, akisema juhudi zao zinaakisi uwezo unaokua wa uongozi barani Afrika. “Kila mmoja wa vijana hawa alichagua huduma badala ya maslahi yake binafsi, jamii badala ya starehe, na maono badala ya hofu. Tunawaheshimu si tu kwa yale waliyofanya, bali pia kwa watu waliogeuka kuwa,” alisema. Bw Kenyatta alisisitiza kuwa uongozi si kuhusu vyeo bali mabadiliko, na kuwataka vijana kutumia vipaji vyao kwa uwazi kuleta athari chanya. Aliongeza kuwa Afrika haina upungufu wa mawazo au nguvu, bali inahitaji uongozi unaojikita katika maadili, unaoongozwa na maono na unaowajibika kwa wananchi. Rais huyo wa zamani alimpongeza Mchungaji Chris Oyakhilome kwa uongozi wake wenye maono na dhamira thabiti ya kuwakuza vijana wa Afrika kupitia Wakfu wa Future Africa Leaders, akisema kuwa ni “jukwaa ambalo halisherehekei mafanikio pekee bali pia linajenga dhamira ya maisha.” Alisifu jitihada za taasisi hiyo kuwekeza katika rasilmali muhimu zaidi Afrika ambayo ni watu wake. Bw Kenyatta pia alitoa shukrani za dhati kwa Rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, aliyemtambua kwa heshima kama “Baba,” kwa uongozi wake wa kudumu na kujitolea kuwaongoza na kuwashauri viongozi chipukizi wa Afrika, jukumu ambalo linaendelea kuunda mustakabali wa bara. “Africa iinuke—ijengwe na Waafrika, iimarishwe na umoja wetu, na iongozwe na viongozi wanaodhamiria kuitumikia,” alisema. Kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka pia alihudhuria hafla hiyo.