WALIMU wakuu wa shule za upili sasa wanataka Wizara ya Elimu kutelekeza mfumo wa kitaifa wa kuteua wanafunzi wa Gredi 10 na kukumbatia mfumo ambapo shule zilisimamia uteuzi huo. Walimu hao wanasema mfumo wa sasa unachanganya na kuondoa uwazi. Wakuu hao, chini ya chama chao (KESSHA), wanasema Mfumo wa Kusimamia Habari za Elimu Kenya (KEMIS) umewazuia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uteuzi, huku shule zikikosa kujua wanafunzi wanaoteuliwa, historia zao za elimu, na uwiano wa maeneo wanayotoka. Haya yanajiri huku wazazi wakiendelea kulalamika kuwa baadhi ya wanafunzi wameteuliwa kujiunga na shule tofauti bila kuomba kuhamishwa. “Awali, tulijua wanafunzi tulioteua, matokeo yao na wanatoka wapi. Kwa mfano, mwanafunzi kutoka Kisauni angepelekwa Murang’a High School, kuhakikisha uwiano wa kitaifa. Sasa tunapata majina tu. Hatujui alama zao au historia zao,” alisema Mwenyekiti wa KESSHA, Willie Kuria. Alieleza kuwa mfumo wa awali, kupitia NEMIS, ulikuwa wenye uwazi na ushirikishaji, ulihakikisha uwiano wa kijiografia na haki sawa katika kaunti zote 47. Alisema wakuu wa shule hawapati matokeo ya Mtihani wa Gredi 9 (KJSEA) ya wanafunzi walioteuliwa kujiunga na shule zao. “Kama mwanafunzi aliye na alama za juu anateuliwa kujiunga na shule za mkoa– tunashangaa. Hatujui kama ufaafu kweli ulifuatwa,” alisema. KESSHA inapendekeza mfumo mseto ambapo wazazi wanaweza kuwasiliana na shule moja kwa moja kupata nafasi, kisha data hiyo iingizwe katika KEMIS kwa idhini ya Wizara ya Elimu. Vilevile, wakuu wanapaswa kupewa nafasi ya kujaza nafasi zinazobaki wanafunzi wakikosa kujiunga na shule walizoteuliwa. Bw Kuria alikanusha madai kuwa wakuu wanadai hongo ili kuteua wanafunzi katika shule bora, akisema pesa zozote zinazotozwa zinatokana na idhini ya Bodi ya Shule (BoM) na risiti rasmi huwa inatolewa.