Kiongozi wa chama cha ODM, Dkt Oburu Oginga, ametangaza kuwa mwaka huu wa 2026 ni wa maamuzi makubwa kwa mustakabali wa chama hicho, akisema maamuzi ya kisiasa yanayofanywa sasa yataamua mwelekeo wa ODM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Dkt Oginga alisema ODM ina chaguo tatu kuu: kuendelea na ushirikiano wake na chama cha UDA cha Rais William Ruto; kuunda ushirikiano mpya wa kisiasa; au kushiriki peke yake kama chama. Alisisitiza kuwa uamuzi huo lazima ufanywe mapema mwaka huu, na si 2027, akionya kuwa kuchelewesha kutazua sintofahamu na migawanyiko ya ndani itakayodhoofisha chama. “Tumesema wazi kuwa tutashiriki uchaguzi ujao kama muungano na vyama vingine , na kama hatutakubaliana basi tunaweza kushiriki peke yetu kama ODM,” alisema Dkt Oginga katika mahojiano ya Mwaka Mpya na redio ya Nam Lolwe FM. “Chaguo zetu ni tatu: kuendelea na serikali jumuishi, kuwa peke yetu au kuunda muungano mpya. Maamuzi haya lazima yafanywe mwaka huu. 2027 ni wa kampeni.” Kauli yake inaweka ODM katika njia panda, takriban mwaka mmoja baada ya marehemu Raila Odinga kuingiza chama hicho katika ushirikiano chini ya serikali jumuishi na utawala wa Kenya Kwanza, hatua iliyobadili kabisa siasa za upinzani nchini. Dkt Oginga alisema uongozi wake unaongozwa na kuheshimu uamuzi wa mwisho wa Raila Odinga kama kiongozi wa ODM. “Tubaki pale Raila alituacha. Alituacha katika serikali jumuishi na Rais Ruto hadi uchaguzi wa 2027,” alisema. Uamuzi huo bado unazua mabishano ndani ya chama. Wakosoaji wanasema ulipunguza nguvu ya ODM kama chama cha upinzani, ilhali wafuasi wanauona kama njia ya kushawishi sera serikalini na kuleta utulivu baada ya maandamano ya muda mrefu. Kuhusu ajenda ya vipengele 10 kati ya ODM na serikali, Dkt Oginga alisema chama kinafuatilia utekelezaji wake. Ajenda hiyo inahusu masuala ya ushirikishaji, ugatuzi, ukaguzi wa deni la umma, uwezeshaji wa vijana, katiba, usawa katika uteuzi wa umma na fidia kwa waathiriwa wa ghasia wakati wa maandamano ya 2017 hadi 2023. “Katika mwaka huu mpya, tunataka kuhakikisha vipengele vyote vinatekelezwa. Baadhi tayari vinaendelea,” alisema. Kuhusu fidia, alisema suala hilo limesimamishwa na mahakama licha ya Wizara ya Fedha kutenga pesa. Akizungumzia jukumu lake baada ya kifo cha Raila Odinga, Dkt Oginga alikiri mzigo ni mkubwa. “Ni viatu vikubwa, lakini ninajaribu kuvivaa. Nahitaji uungwaji mkono wa walio karibu nami,” alisema, akiongeza kuwa wafuasi wa ODM mashinani wameonyesha mshikamano. Alikanusha madai kuwa mkutano wake wa hivi majuzi katika makazi ya Rais Ruto huko Kilgoris ulikuwa wa kuunda njama. Alisema ulikuwa mkutano wa kawaida wa kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Rais. “Hatuna siri. Tuko katika serikali jumuishi. Tunaweza kukutana au kuzungumza kwa simu,” alisema.