WATU 16 walifariki ndani ya saa 72 na wengine wengi kujeruhiwa huku ajali mbili za barabarani zikitokea licha ya msako mkali wa mashirika mbali mbali kudumisha usalama barabarani. Katika ajali ya kwanza, matatu iliyokuwa ikielekea Mombasa iligongana na basi lililokuwa likiekekea Nairobi, ambapo watu wanane walifariki na tisa kujeruhiwa.Ajali hiyo ilitokea eneo la Konza usiku wa kuamkia jana. Matatu ya kubeba abiria18 inayosimamiwa na Naekana Sacco, ilikuwa inaelekea Lungalunga katika Kaunti ya Kwale kupitia Mombasa ajali ilipotokea. Manusura walipelekwa hospitali ya Rufaa ya Machakos kwa matibabu. Wanaume watatu na wanawake watatu walifariki papo hapo, huku wanaume wawili wakifariki wakipokea matibabu katika hospitali hiyo. “Hospitali ya Machakos Level 5 ilipokea wagonjwa 11 waliojeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani,” alisema Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Machakos, Rashid Kalla, katika taarifa jana. Alisema hospitali ilitoa huduma kwa wagonjwa watano kati ya tisa waliokuwa na majeraha madogo.Kamanda wa polisi eneo la Mukaa, Hussein Abduba alisema uchunguzi wa awali ulionyesha matatu ilikuwa inajaribu kupita lori ilipogongana na basi. Katika ajali ya pili, matatu nyingine iligongwa kutoka nyuma na lori kisha ikagonga lori lililokuwa mbele yake. Kulingana na maafisa wa polisi, ajali hiyo ilitokea eneo la Kikopey katika barabara ya Gilgil-Nakuru ambapo watu watano walifariki. Kamanda wa Polisi wa Gilgil, Winsone Mwakio, alithibitisha tukio hili na kusema kuwa watu 5 waliaga na wengine sita kujeruhiwa.Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) ilisema katika taarifa kuwa inahuzunishwa sana na ajali hizi za barabarani. “Tunawaomba watumiaji wote wa barabara kuchukua tahadhari kubwa na kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa wakati watoto wetu wanaporejea shuleni wiki ijayo,” iliongeza NTSA.