Serikali yabuni mwongozo wa kuongeza ‘ladha’ chai ya Kenya

Serikali imeanzisha miongozo kadhaa inayolenga kuongeza mapato ya wakulima wadogo wa chai kutoka Sh50.18 kwa kilo moja ya majani ya chai hadi Sh100 kufikia mwaka 2027. Wakulima wote nchini watanufaika na ongezeko hili la mapato, bila kujali mahali wanapozalisha chai yao. Hatua hii ya serikali inajibu wasiwasi wa viongozi kutoka Kisii, Nyamira, na Bonde la Ufa Mashariki na Magharibi, ambao walilalamika kuhusu bonasi kwa wakulima wa chai. Mwezi Novemba mwaka jana, viongozi hao walimwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, wakilalamikia ukosefu wa usawa katika bonsai. Walilalamika kwamba tofauti ya bei ya chai katika maeneo mbalimbali ya Kenya inahitaji kuchunguzwa. Hali hii ilipelekea Kamati ya Kilimo ya Bunge la Kitaifa kufanya uchunguzi, uliobaini kuwepo kwa tabia zisizo za ushindani katika sekta ya chai, ambazo zinachangia kushuka kwa bei ya chai na kusababisha mapato duni kwa wakulima. Katika ripoti kwa Bunge, Waziri wa Kilimo, Mutahi Kagwe, alieleza kwamba miongozo inatarajiwa kuanza kutekelezwa kikamilifu kufikia mwezi Juni mwaka huu. Miongozo hiyo iliandaliwa na kamati ya mashirika mengi, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Bodi ya Chai ya Kenya (TBK), Shirika la Utafiti la Chai (TRF), viwanda vya chai na wafanyabiashara. Sehemu yake inaweka kiwango cha chini cha ubora wa majani chai yanayohitajika kutumiwa na viwanda vyote vya chai. Mara baada ya kutekelezwa, utasaidia kuondoa tofauti za ubora na bei kati ya maeneo ya magharibi na mashariki ya Kenya. Waziri Kagwe alieleza Bunge kwamba serikali pia inaanzisha maabara jijini Mombasa ili kuchunguza na kuthibitisha ubora na usalama wa chai. Aliambia wabunge kwamba ujenzi wa maabara umekamilika, na mchakato wa kuweka vifaa unaendelea. Inatarajiwa kumalizika kufikia Juni mwaka huu, ili kuwezesha kuanza kazi. Maabara hiyo itahusika na uchunguzi wa ubora na usalama wa chai kupitia vipimo vya kisayansi vya chai, Aidha, kupitia maabara hiyo, Bodi ya Chai ya Kenya itafanya tathmini ya chai kama sehemu ya shughuli za kudhibiti ubora katika kuamua bei. Katika mwongozo wake wa tatu, serikali itatekeleza mipango mikakati ya kuboresha ubora wa chai, hasa kwa viwanda vya chai vya Magharibi ya nchi, ili kuboresha ubora na kufikia mahitaji ya soko. Serikali pia itatoa mikopo ya Sh3.7 bilioni kwa viwanda vya chai vidogo kwa kiwango cha riba cha asilimia 5 kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Kenya ili kusaidia viwanda vya chai kuimarisha vifaa na mashine katika viwanda vidogo vya chai. Pia inatarajiwa kwamba viwanda vitatumia mikopo hii kuboresha uzalishaji wa chai ambayo hupata bei nzuri katika masoko maalum. Shirika la Maendeleo ya Chai la Kenya (KTDA) pia limejitolea kuwekeza katika uboreshaji wa viwanda na nishati ili kupunguza gharama. Ili kupunguza gharama za uzalishaji katika viwanda vya chai, Bodi ya Chai ya Kenya imeanzisha ukaguzi wa kifedha na usimamizi katika viwanda vya chai ili kubaini ikiwa kuna matatizo yoyote katika usimamizi wa viwanda ambayo yanaweza kuathiri mapato ya wakulima.