Mwanzo mgumu shule zikifunguliwa kwa muhula wa kwanza

SHULE zinapofunguliwa wiki hii kuanza kalenda ya masomo ya 2026, sekta ya elimu inajiandaa kwa mwanzo mgumu zaidi kuwahi kushuhudiwa, huku kukiwa na mvutano kuhusu karo, uhaba wa walimu na miundombinu. Kwa mara ya kwanza, wanafunzi wa kwanza 1.13 milioni chini ya mfumo wa Elimu unaotegemea Umilisi (CBE) wanapanda ngazi hadi shule za Sekondari Pevu (Gredi ya 10), hatua inayohitimisha safari ya mageuzi ya elimu iliyodumu kwa muongo mmoja. Hata hivyo, kile kilichotarajiwa kuwa hatua ya kujivunia tayari kimegubikwa na sintofahamu kuhusu uteuzi wa wanafunzi, upungufu wa miundombinu na uhaba mkubwa wa walimu, hali iliyowaacha wazazi, walimu wakuu na wanafunzi wakiwa na wasiwasi. Ili kuleta utulivu katika mpito huo, serikali imetoa Sh44 bilioni kama mgao wa muhula wa kwanza. Shule za Sekondari za Kutwa zitapokea Sh26 bilioni, Shule za Msingi za Kutwa Sh14 bilioni huku Elimu ya Msingi Bila Malipo ikitengewa Sh3.7 bilioni. Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba, aliwaonya walimu wakuu dhidi ya kutoza ada za ziada, akisema baadhi yao wamekuwa wakitoza gharama fiche za chakula na miundombinu. “Wakuu wa shule wahakikishe matumizi bora ya rasilmali hizi za umma na waache mara moja kutoza ada au michango ya ziada. Tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayepatikana akikiuka maagizo haya,” alisema Bw Ogamba. Kwa upande wao, wakuu wa shule wanasema changamoto kubwa bado ni ufadhili, kwani viwango vya karo vilivyowekwa 2014 haviambatani na hali ya sasa ya gharama. Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA), Bw Willie Kuria, alisema kupungua kwa idadi ya wanafunzi baada ya darasa moja kuhamishiwa shule za msingi kumeathiri mapato ya shule huku gharama zikiendelea kuwa juu.