Tume ya Madini yaja na mkakati wa ushirikishwaji wa wazawa

Dodoma. Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, ambapo Tume ya Madini mara kwa mara itatangaza orodha ya bidhaa zitakazotolewa na kampuni za Kitanzania, huku bidhaa 20 zikiainishwa. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amewaambia waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Jumatatu Januari 5, 2026, kuwa kanuni ya 13A katika marekebisho hayo inataja orodha ya bidhaa na huduma ambazo zinatakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania. Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini kwa manufaa ya taifa. Awamu ya kwanza ilikuwa Novemba 14, 2025, ambapo Tume ya Madini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100. “Ndugu wanahabari, nitumie nafasi hii kutoa rai kwa Watanzania kuhakikisha wanapata utaalamu sahihi unaohitajika katika shughuli za madini, ili wawe miongoni mwa wanaostahili kupatiwa fursa za ajira katika migodi, sambamba na fursa za utoaji huduma katika miradi hiyo,” amesema Mavunde. Waziri ameagiza watoa huduma wote kuhakikisha wanatoa huduma bora kulingana na viwango stahiki ili kuendelea kuaminika katika utoaji wa huduma husika. Katika hatua nyingine, ametaja siri ya mafanikio ya kuongeza mapato ndani ya wizara kuwa inatokana na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi na ulazima wa wafanyabiashara kuuzia madini katika masoko. Amesema wizara ina vituo 103 vya ununuzi na masoko 44, ambapo mauzo yameongezeka kutoka Sh526.722 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.071 trilioni mwaka 2024/25, huku lengo la mwaka 2025/26 likiwa kukusanya Sh1.2 trilioni. Kwa mujibu wa waziri, lengo la makusanyo kwa mwaka 2025/26 ni Sh1.2 trilioni, sawa na Sh100 bilioni kwa mwezi. Mchimbaji wa madini katika machimbo ya dhahabu Nzuguni, Luzwilo Majebele, amesema kizuizi kimekuwa kikubwa katika uuzaji wa madini hayo, kwani hata vipande vidogo hawaruhusiwi kuuza bila utaratibu wa kisheria. Majebele amesema awali kulikuwa na mpango wa kuuza madini kwa njia ya udalali katika machimbo hayo, lakini sasa wanatakiwa kununua kutoka kwa wenye leseni, katika vituo maalumu.