Hakuna kucheka na mtu, asema Ruto akizindua mikakati ya kuangamiza ulevi

RAIS William Ruto Jumatano, Januari 7, 2026 aliongoza kikao cha mashirika mbalimbali kuweka mikakati ya kuimarisha vita dhidi ya ongezeko la matumizi ya pombe na dawa za kulevya pamoja na changamoto za usalama zinazohusiana na tatizo hilo. Katika utekelezaji wa vipaumbele alivyotoa katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, Rais aliagiza kuharakishwa kwa hatua za kisheria, kitaasisi na kiutendaji ili kukabiliana na matumizi ya pombe na dawa za kulevya kama suala la maendeleo ya taifa na usalama. Kulingana na taarifa kutoka Ikulu, Rais alitilia mkazo utekelezaji wa sheria na kusaidia waathiriwa. “Kikao hicho kilikubaliana kuwa mfumo husika wa kisheria utakamilishwa ndani ya siku 10 zijazo ili kuimarisha uratibu, utekelezaji wa sheria na uwajibikaji miongoni mwa taasisi za serikali,” ilisema taarifa kutoka Ikulu kwa vyombo vya habari. Waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Katibu Raymond Omollo, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Naibu Inspekta Jenerali Eliud Lang’at na Gilbert Masengeli, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohammed Amin, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) Stephen Mairori na Afisa Mkuu Mtendaji Anthony Omerikwa, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa KEBS Esther Ngari. Rais aliagiza kuanzishwa kwa vituo vya kurekebisha tabia katika kaunti zote 47, NACADA ikishirikiana kwa karibu na serikali za kaunti kuhakikisha vituo hivyo vinafanya kazi kikamilifu na vinapatikana kwa wananchi. Hospitali za rufaa za kitaifa pia zitawezeshwa kuanzisha vituo vya urekebishaji tabia ili kuimarisha huduma maalum za matibabu na ushauri nasaha. Ili kuvuruga zaidi mitandao ya ulanguzi na uhalifu wa kupangwa, kikao hicho kiliazimia kuunda kikosi cha mashirika mbalimbali katika vituo vitano muhimu vya mipakani nchini, hatua itakayoboresha ufuatiliaji, ushirikiano wa kijasusi na utekelezaji wa pamoja.