MAONI: Ajabu Waafrika kuomba viongozi wao watekwe na Amerika kama Maduro?

SIKUJUA Waafrika wanawachukia viongozi wao kupindukia hadi hivi majuzi Amerika ilipomteka Rais wa Venezuela, Nicholas Maduro, kutoka jijini Caracas na kumsafirisha usiku wa manane hadi jijini New York. Hatimaye, Maduro alishtakiwa kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya nchini Amerika, miongoni mwa makosa mengine ambayo kwa maoni yangu ni visingizio vinavyonuiwa kumharibia jina mbwa kabla ya kumnyonga, chambilecho Waingereza. Amerika nayo inatuhumiwa kwa kuyamezea mate mafuta mengi yanayopatikana Venezuela, jambo lililoniwia vigumu kuitetea, hata kabla ya Rais Donald Trump kuringa jinsi atakavyoyauza na ‘kuzinufaisha nchi zote mbili’. Tangu ianze kadhia nzima ya rais wa watu kutekwa na kugeuzwa mshukiwa hatari katika muda wa saa chache, Waafrika wengi wamekuwa wakihimiza Amerika - baadhi yao kwa matani na wengineo kwa kuaminia kabisa - kwamba inapaswa kutua kwao na kuondoka na watawala wao usiku wa manane. Waganda waliuliza kwa nini Amerika haikuanzia na kiongozi wao, Yoweri Museveni, Watanzania wakabeza eti ‘Kimama’ Samia Suluhu Hassan hapati hata lepe la usingizi kwa kuhofia kujiwa bila taarifa, Wakenya wakajiuliza kwa nini maandamano ya kizazi cha Gen - Z hayakufanyika wakati kama huu ambapo Rais Donald Trump yupo madarakani ili amjie Rais William Ruto upesi. Wanigeria walijipa moyo kwamba, hata baada ya ndege za kivita za Amerika kumsaza Rais Bola Ahmed Tinubu zilipoangusha mabomu nchini kwao zikiwalenga magaidi, kuna matumaini kuwa mtawala wao huyo anaweza kutekwa na kusafirishwa hadi Amerika ili akajibu mashtaka ya ufisadi na mengineyo. Swali ambalo nimekuwa nikijiuliza ni, kwa nini Waafrika wengi wanataka viongozi wao watekwe na Amerika, kwa makosa gani yanayoliathiri taifa hilo tajiri moja kwa moja? Pia nimejiuliza watawala wanaochukiwa kiasi hicho walijipataje katika nyadhifa hizo ikiwa si kuchaguliwa na wananchi wenyewe. Ajabu akidi ni kwamba, miongoni mwa watawala wanaopendekezwa kutekwa, hakuna hata mmoja ambaye aliingia madarakani kwa mtutu wa bunduki. Waliopindua serikali zao na sasa wanazitawala watakavyo wamenyamaziwa tu; wanaokipata ni hao tuliowachagua wenyewe. Kimsingi, tunawataka Waamerika waje Afrika kufagia uchafu tulioleta kwa hiari yetu wenyewe, au uliotushinda kuzoa. Kuna hakika gani kwamba hawa tulionao wakitekwa hatutawachagua wengine wabaya zaidi? Kwani hatujui viongozi tunaojichagulia wanaakisi hali halisia ya nchi na jamii zetu? Yaani mtu amekulia kwenu mtaani kwenye wezi, malaya na wacheza-kamari, lakini unataka awe mweupe kama pamba ilhali una hulka yake pia. Haiwezekani! Hivi mapenzi kati ya watawala na watawaliwa yanaisha haraka namna hiyo kwa nini? Labda tunawaonea wivu, sisi wenyewe ni mahasidi wasio na sababu, eti tunatamani kuona wakiteswa na Mwamerika ilimradi tu? Kumbuka awali sisi ndisi tu tuliopaza sauti kwa vinywa vipana na kusema Amerika si polisi wa dunia eti iingilie kila mzozo duniani, au izikomeshe tawala dhalimu. Nakubaliana na mtazamo kwamba viongozi wengi wa Afrika na mataifa yanayoendelea kwa jumla hawafai kuwa madarakani kwa kuwa ni majambazi waliovalia suti na tai tu. Yupo anayevaa buibui na mitandio, hapa karibu na kwetu. Tunachopaswa kuelewa kama Waafrika ni kwamba jukumu la kuleta utawala bora ni letu wenyewe na wala si la Waamerika. Mataifa yote yaliyoendelea, hasa yaliyo mbioni kushindania ushawishi wa kimataifa, yanajali na kulinda maslahi yao pekee. Maslahi hayo yakihatarishwa, basi mataifa hayo huchukua hatua kali na za dharura mno hata ikiwa yatahatarisha maslahi yetu katika mchakato huo. Serikali ya Amerika hasa haipendi mchezo katika masuala ya usalama wa kitaifa na uuzwaji wa dawa za kulevya nchini mwake, na ndiyo sababu inawakamata na kuwafunga jela viongozi wa magenge ya usafirishaji wa mihadarati kutoka pembe zote za dunia. Mkenya, mara ya mwisho ulipowasikia wana wa marehemu bwanyewe na mlanguzi mkuu wa mihadarati, Ibrahim Akasha, wakihangaisha watu Afrika Mashariki ni lini? Walikamatwa Kenya na kusafirishwa moja kwa moja hadi Amerika, wakafungwa jela upesi kwa kujaribu kuuza bidhaa zao hizo huko. Tunaweza kuuana tunavyotaka, lakini tusiguse chochote ambacho Amerika inakitaka, kukitamani au kukimiliki. Ni kwa sababu hii ambapo husikii Amerika ikilaani ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea ndani ya mataifa inayoshirikiana nayo katika biashara ya mafuta na shughuli za kijeshi, hasa ya Mashariki ya Kati. Viongozi wengi Afrika ama ni washirika wa Amerika katika mambo mengi au wanaiogopa kiasi cha kutothubutu kugusa maslahi yake, hivyo matamanio yako kwamba watekwe na kushtakiwa kama Rais Maduro ni dua ya kuku isiyompata mwewe. Badala ya Waafrika kujaa chuki mioyoni na kutia dua kimya-kimya kwamba Amerika iwaondolee mzigo wa utawala mbaya, hebu na tuanzie kwa kupalilia demokrasia na kutumia akili sawasawa tunapopiga kura. - Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika (mutua_muema@yahoo.com)