KWA mwaka wa pili mfululizo, idadi ya wasichana ilizidi wavulana katika Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE), jambo linaloonyesha mabadiliko ya kijamii na kielimu yanayoendelea kushuhudiwa nchini, hasa katika ushiriki wa wasichana katika elimu ya sekondari. Takwimu rasmi za Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) zinaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 993,226 walifanya mtihani wa KCSE mwaka 2025, ikilinganishwa na watahiniwa 962,512 mwaka 2024. Hii ni sawa na ongezeko la watahiniwa 30,714, au asilimia 3.19. Ongezeko hili linaashiria kuimarika kwa wanafunzi katika shule za upili pamoja na juhudi za serikali na wadau wa elimu kuhakikisha watoto wanabaki shuleni hadi kumaliza masomo ya sekondari. Kati ya watahiniwa wote wa mwaka 2025, wavulana walikuwa 492,012 (asilimia 49.54), huku wasichana wakiwa 501,214 (asilimia 50.46). Hii ni mara ya pili mfululizo tangu kuanzishwa kwa mtihani wa KCSE ambapo idadi ya wasichana imezidi ile ya wavulana, ishara kuwa juhudi za kuhimiza elimu ya mtoto wa kike zinaanza kuzaa matunda. Hata hivyo, hali hiyo haikuwa sawa kote nchini. Kaunti kumi zilirekodi idadi kubwa ya wavulana kuliko wasichana. Kaunti hizo ni pamoja na Garissa, ambako wavulana walikuwa asilimia 66.24 dhidi ya wasichana asilimia 33.76, Mandera (65.09 dhidi ya 34.91), Wajir (60.10 dhidi ya 39.90), Turkana (57.67 dhidi ya 42.33) na Narok (53.10 dhidi ya 46.90). Kaunti nyingine ni Samburu, Mombasa, Homa Bay, Nyamira na Pokot Magharibi. Hali hii imehusishwa na changamoto za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni zinazoathiri elimu ya wasichana katika maeneo hayo. Kwa upande mwingine, kaunti 14 zilikuwa na idadi kubwa ya wasichana kuliko wavulana. Kaunti hizo ni pamoja na Vihiga, Elgeyo Marakwet, Kisumu, Kiambu, Kwale, Nairobi, Kakamega, Meru, Isiolo, Uasin Gishu, Machakos, Kitui, Busia na Tharaka Nithi. Wataalamu wa elimu wanasema hali hii inaonyesha mafanikio ya sera za elimu jumuishi na kampeni za kuzuia wasichana kuacha shule. Kaunti 23 zilirekodi uwiano wa karibu sawa wa kijinsia, zikionyesha usawa mkubwa kati ya wavulana na wasichana. Kaunti hizo ni pamoja na Lamu, Marsabit, Embu, Tana River, Laikipia, Kisii, Baringo, Migori, Trans Nzoia, Nandi, Kajiado, Taita Taveta, Kericho, Siaya, Kilifi, Bomet, Nyeri, Nyandarua, Murang’a, Nakuru, Kirinyaga, Bungoma na Makueni. Kuhusu umri wa watahiniwa, idadi ya wanafunzi wenye umri wa miaka 16 na chini iliongezeka kutoka 20,546 mwaka 2024 hadi 26,391 mwaka 2025, sawa na asilimia 2.65 ya watahiniwa wote. Hata hivyo, idadi kubwa zaidi ya watahiniwa, 716,048 (asilimia 72.02), walikuwa katika umri ufaao wa kati ya miaka 17 na 19. Uchambuzi wa kijinsia unaonyesha kuwa wasichana walifanya vyema zaidi kuliko wavulana katika masomo sita: Kiingereza, Kiswahili, Lugha ya Ishara ya Kenya, Sayansi ya Nyumbani, Elimu ya Dini ya Kikristo (CRE) na Sanaa na Ubunifu. Wavulana, kwa upande wao, waliongoza katika masomo 11, yakiwemo Hisabati, Baiolojia, Kemia, Sayansi ya Jumla, Historia na Serikali, Jiografia, Elimu ya Dini ya Kiislamu, Ujenzi na Masomo ya Biashara.