Siasa za ubabe: Wamuchomba aponda Gachagua adai ni mbaguzi wa akina mama

MBUNGE wa Githunguri, Bi Gathoni Wamuchomba, amemshambulia vikali aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kufuatia madai ya vitisho na shinikizo za kisiasa. Bi Wamuchomba alimtuhumu Bw Gachagua kwa kudaiwa kumtisha na kumlazimisha mara kwa mara aondoke katika Chama cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga na Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP). “Sasa Wamunyoro anajaribu kunitisha kwa kunilazimishwa kupitia mashambulizi ya mara kwa mara nijiunge na DCP. Ninalazimika kuweka wazi ukweli kwake,” aliandika Mbunge huyo kwenye ukurasa wake wa X mnamo Jumatatu January 5. Akieleza hasira zake kupitia mtandao wa X, Jumanne Januari 6, 2026, Bi Wamuchomba alimtaja Bw Gachagua kama mtu anayewachukia wanawake, akitaja matukio kadhaa anayodai yanaonyesha dharau yake kwa viongozi wa kike. “Wamunyoro ni mwenye chuki dhidi ya wanawake. Wakati wa hoja ya kumng’atua, wabunge wawili wanawake walidai hadharani kuwa aliwatukana kwa maneno yasiyofaa kuchapishwa,” alisema Bi Wamuchomba. Kwa mujibu wa mbunge huyo, aliyekuwa Naibu Rais anadaiwa kutumia baadhi ya washirika wake wakuu kuwatisha wanasiasa wa Mlima Kenya waliokataa kujiunga na chama hicho cha upinzani. Bi Wamuchomba aliwatuhumu Seneta wa Nyandarua, John Methu na Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa kwa madai kuwa vibaraka wanaotumiwa na Gachagua kuwatisha viongozi wanaounga mkono serikali katika eneo la Mlima Kenya. “Anamtumia Seneta Karungo kuwadharau wale wasio katika chama cha ‘Mlima’. Karungo bado ni Seneta wa UDA lakini anapiga kelele kuhusu chama kingine,” alisema. Aliongeza: “Kama chama hiki kina nguvu kweli, kwa nini Methu, Karungo na Nyutu wasijiuzulu kwanza, halafu tuwachague tena kupitia chama chao kipya cha ‘masikio’? Sijiungi na chama hicho, nitasalia UDA hadi 2027.” Katika kauli yake, Mbunge huyo alisema si mara ya kwanza kukumbana na vitisho kama hivyo kutoka kwa Bw Gachagua, akiongeza kuwa mwaka 2023 alipitia hali kama hiyo baada ya kupiga kura dhidi ya Mswada wa Fedha. Bi Wamuchomba, ambaye hapo awali alikuwa mfuasi sugu wa Bw Gachagua, sasa ameibuka kuwa mmoja wa wakosoaji wake wakubwa, akimlaumu kwa kukosa nidhamu kisiasa.