MKUFUNZI mpya wa Bandari, Benard Mwalala, alianza kazi kwa kishindo akiwaongoza kupepeta Kakamega Homeboyz 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu (KPL) iliyochezewa uwanja wa Mbaraki, Mombasa, jana. Mwalala alitangazwa rasmi kurejea Bandari jana baada ya kumalizika kwa vuta ni kuvute kati yake na Shabana ambako alikuwa akihudumu kama naibu kocha. Alitua Mombasa baada ya timu hizo mbili kuelewana kuhusu malipo na sasa mashabiki wa Bandari wana matarajio makubwa kwamba atasaidia kubadilisha matokeo mabaya ya timu hiyo ya Pwani. Tangazo rasmi la kurejea kwake lilitua kupitia barua rasmi iliyotiwa sahihi na Meneja Mkuu wa Bandari, Tony Kibwana. Mwalala anachukua nafasi ya raia wa Morocco, Mohamed Borji, aliyetimuliwa baada ya kuwa usukani kwa majuma machache tu mwezi uliopita. Borji naye alikuwa amevaa viatu vya Ken Odhiambo aliyefurushwa miezi kadha iliyopita kufuatia msururu wa vichapo. Mwalala aliongoza Bandari kuzoa Kombe la Shirikisho la Soka Nchini (FKF Cup) mnamo 2019. Vile vile, alikuwa usukani Bandari iliposhiriki Kombe la Mashirikisho ya Soka Afrika CAF Confederations Cup) mwaka uo huo, wakabanduliwa na Horoya AC ya Guinea. Jana aliwasili na kismati Bandari ilipotoka nyuma kuilaza Homeboyz katika ushindi wao wa kwanza wa mwaka huu mpya. Oliver Machaka alikuwa ameweka Homeboyz kifua mbele dakika ya 58. Bandari ilijizatiti na hatimaye ikasawazisha katika dakika ya 91 kupitia Mohamed Barisa. Wakapata motisha na dakika ya 95 Amza Ngamchia alitinga goli la pili na la ushindi. Kufuatia kichapo Homeboyz wapo nafasi ya tatu kwa alama 24 baada ya kusakata mechi 16. Nao ushindi ulifanya Bandari kufunga orodha ya 10-bora na alama 20 wakiwa wamewajibika michuano 15. Kwenye mechi zingine zilizogaragazwa jana, APS Bomet ambao wapo msimu wao wa kwanza KPL, walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Mara Sugar kwenye uwanja wa Kericho Green Bomet. Mathare United nao walishindwa kutumia vyema uga wao wa nyumbani wa Kasarani Annex wakipigwa 2-0 na wageni Murang’a Seal. Uwanjani Annex, kocha wa Murang’a Seal Osborne Monday aliwaongoza vijana wake kudumisha rekodi nzuri ya kutopoteza kwenye mechi 10 hadi sasa. Victor Haki na Jackson Imbakiah walifunga mabao hayo mawili na kuwapa Seal ushindi huo. Baada ya kujibwaga uwanjani mara 15, Seal wana alama 21 kwenye nafasi ya nane. Mathare United ambao ni mabingwa wa 2008, itabidi wajikakamue kwa sababu wanashikilia nambari 13 kwa alama 18 baada ya mechi 16. Francis Omondi alifungia limbukeni APS Bomet naye Robinson Musungu akacheka na nyavu upande wa Mara Sugar ugani Kericho. Sare hiyo hata hivyo imeacha APS Bomet pabaya, wakiwa nambari 16 kwa alama 14 baada ya mechi 15. Mara Sugar wapo nambari 12 kwa alama 19 baada ya mechi 15.