MATOKEO ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) 2025 yamefichua shule ndogo ambazo hazikujulikana sana awali, baada ya kupata wastani alama bora na kushinda shule zilizokuwa zikichukuliwa kama mabingwa kitaifa. Shule za jadi kama Alliance High School, Kenya High School, Mang’u High School na Kapsabet Boys High School bado zinaendelea kutawala, lakini sasa zinakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa shule mpya, ndogo na za kibinafsi. Shule hizo ni kama Nova Pioneer Tatu Boys High School ya Kaunti ya Kiambu, iliyopata wastani wa alama 10.2 kutoka 8.3 mwaka 2024. Kati ya watahiniwa 82, wanafunzi 24 walipata A-, 49 B+, wanane B na mmoja B-. Asilimia 100 ya wanafunzi walifuzu kujiunga na vyuo vikuu, kulingana na Kaimu Mwalimu Mkuu Andrew Meraba. Shule ya Pangani Girls ilipata wastani wa 9.718 na kuimarisha sifa yake kama moja ya shule bora nchini. Ilikuwa na alama 39 za A, wanafunzi 92 wakipata A-, 101 B+, 69 B, 44 B-, 17 C+, wanane C, sita C- na mmoja D+. Katika Kaunti ya Kajiado, Shule ya Wasichana ya Ghanima El-Marzuq, Isinya, iliongoza miongoni mwa shule za kibinafsi.