Kahiga amruka Gachagua, asema anaunga Ruto na UDA

GAVANA wa Nyeri Mutahi Kahiga ambaye amekuwa mwandani wa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ametangaza kuwa bado yuko UDA wala hajahamia chama kingine kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Kahiga amekuwa kati ya wanasiasa ambao hujitokeza mara kwa mara kumtetea Bw Gachagua na kuishambulia serikali ya Rais William Ruto kwa kumhangaisha. Mnamo Alhamisi wiki jana, alikuwa na Bw Gachagua mjini Nyeri ambapo walihutubia mkutano wa kisiasa, wengi wakikisia ashajiunga na DCP. “Mimi bado niko UDA na huwezi kubadilisha hilo,” akasema akiwahutubia waumini katika Kanisa la St Paul Kariki, eneobunge la Othaya, Kaunti ya Nyeri, Jumapili, Januari 11, 2026. Ibada katika kanisa hilo pia ilihudhuriwa na Rais Ruto, naibu wake Prof Kithure Kindiki na viongozi wengine wa serikali. Bw Kahiga alitumia jukwaa hilo kuwataka Wakenya watofautishe siasa na masuala ya uongozi akisema kwa sasa anamakinikia kutimiza ajenda yake ya maendeleo kwa wakazi wa Nyeri. “Siku za kupiga siasa zitakuja lakini kwa sasa sote tumuunge mkono Rais Ruto ili afanye kazi yake,” akasema Bw Kahiga. Bw Kahiga pia alisema viongozi ambao wanamuunga mkono Rais Ruto wana haki ya kufanya hivyo hadharani. “Nilimpigia Ruto kura, yeye ni rais wangu na mimi ni gavana. Sijui kwa nini baadhi ya watu wanachanganyikiwa? Bado nina rais,” akaongeza Bw Kahiga akishangiliwa na waumini. Kiongozi huyo alisisitiza kuwa ni jukumu lake la kikatiba kufanya kazi na serikali ya kitaifa na kumlaki Rais kila mara anapozuru kaunti hiyo.