NAIBU Mkuu wa Utumishi wa Umma na Mkuu wa Utekelezaji Miradi ya Serikali katika Afisi ya Rais Eliud Owalo amejiuzulu . Katika chapisho kwenye kurasa zake za mitandaoni, Bw Owalo ambaye amekuwa mshirika wa karibu wa Rais William Ruto kutoka Nyanza anasema anataka kuwania urais, na kwa sababu hiyo, haingewezekana kwake yeye kuendelea kushikilia wadhifa huo. Bw Owalo ni naibu wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei na ni mmoja wa wanasiasa kutoka Nyanza walioanza kufanya kazi na Rais Ruto mapema mno, hata kabla ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kushirikiana na Rais kuunda Serikali Jumuishi.