Mahangaiko ya karo wanafunzi wakianza kujiunga na Gredi 10

JUMLA ya wanafunzi milioni 1.13 wanajiunga na Shule za Sekondari Pevu leo huku nyingi za shule hizo zikikumbwa na uhaba wa walimu na vifaa hitajika. Imebainika kuwa idadi kubwa ya shule hizo hazina walimu wa kutosha kufundisha masomo yaliyomo kwenye mikondo mitatu ya Mtaala wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBE). Mifumo hiyo ni; Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), Sayansi ya Jamii na Spoti na Sanaa. Mbali na hayo, wazazi wa wanafunzi watakaojiunga na shule hizo kuanzia leo wanalalamikia ukosefu wa pesa za karo na zile za kugharimia ununuzi wa vitu ambavyo watoto wao wanahitaji kuripoti navyo shuleni. Baadhi ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na shule za Sekondari Pevu kwa masomo ya Gredi ya 10 walisimulia jinsi ambavyo uchechefu wa hela unavyoweza kuwazuia kuingia shuleni. Elosy Mwendwa aliyekuwa mwanafunzi wa Gredi 9 katika Shule ya Thinyaine Junior iliyoko Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru alipata alama 63 yuko katika hatari hiyo. Kulingana na mamake, Vierina Nkirote, bintiye ameitwa katika Shule ya Upili ya St Mary’s Girla, Meru lakini wameshindwa kumudu karo na pesa za kumnunulia mahitaji mengine. “Huwa tunategemea kilimo kupata karo ya watoto wetu. Hata hivyo, msimu huu, mimea yetu imeathiriwa na kiangazi. Sasa ombi letu ni kwamba binti yangu apate mhisani kufadhili masomo yake,” mama huyo alisema. Katika muhula wa kwanza familia hiyo inahitaji Sh26,000 za karo kando na pesa za kununulia mahitaji mengine kama sare za shule. Kaunti ya Kirinyaga, Prais Mawia huenda asijiunge na Shule ya Upili ya Wasichana ya Alliance aliyoitamani kutokana na ukosefu wa karo. Licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi, mwanafunzi huyo alifanya vizuri katika mtihani wa KJSEA kwani alikuwa mwanafunzi bora zaidi katika Sekondari Msingi ya Kimbimbi, Kirinyaga baada ya kupata alama 65 kati ya 72. Sasa mzazi wake, ambaye hufanya kazi ya vibarua anasema hawezi kupata Sh53,535 zinazohitajika kama karo ya mwaka mmoja. Naye Stephanie Wanjeri ambaye alifanya mtihani wa KJSEA katika shule ya msingi ya Muthiria iliyoko kaunti ya Murang’a huenda akakosa kujiunga na shule ya upili kwa ukosefu wa pesa. Wanjeri alipata alama 65 kati ya 72 na akaitwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Ngandu anakohitaji kulipa karo ya Sh55, 000 kwa mwaka. Hata baada ya kuahidiwa basari ya Sh5,000 familia yake haiwezi kugharamia pesa zilizosalia. Katika Kaunti ya Bomet, ndoto ya Mercy Chepkemoi ya kujuiunga na Shule ya Upili ya Kapolesero huenda isitimie. Hii ni kwa sababu babake, ambaye ndiye mlezi wake wa kipekee baada ya mamake kufa, hawezi kumudu karo yake. Chepkemoi alipata alama 35 katika mtihni wa KJSEA lakini sasa babe, Joseph Kiprotich Korir, hawezi kupata Sh16,000 zinazohitajika katika muhula wa kwanza katika Shule ya Upili ya Kapelesero.