Raia Venezuela wajaa imani kwamba Amerika itainua uchumi wao baada ya kunyaka Maduro

BAADA ya uvamizi wa Amerika uliomwondoa mamlakani Rais Nicolas Maduro, raia wanaamini kuwa mazungumzo kuhusu kuuzwa kwa mafuta Amerika kutaimarisha hali yao kiuchumi. Wanajeshi wa Amerika waliwashangaza wengi waliposhambulia Caracas kwa mabomu usiku na wakamnasa Maduro majuma mawili yaliyopita. Lakini wachanganuzi wanaamini kuwa uvamizi huo umebadilisha pakubwa hali ya nchi hiyo na kuleta matarajio ya kuimarika kwa uchumi. Mrithi wa Maduro, kiongozi wa muda Delcy Rodriguez amesisitiza kuwa Venezuela sio “mtumwa” wa Amerika baada ya kumnasa rais wao. Hata hivyo, alikubali kushirikiana na Amerika katika biashara ya mafuta. Chini ya utawala wa Maduro, wananchi walilalamikia mfumko wa bei na kupungua kwa mapato kutoka mataifa ya kigeni kutokana ukosefu wa uwekezaji.