MADAKTARI zaidi ya 50 kutoka nchini ya DR Congo wamemshtaki Waziri wa Afya Aden Duala kwa kutoa maagizo wanyimwe leseni kuhudumu humu nchini. Madaktari hao wanaomba Mahakama kuu ya Milimani ibatilishe uamuzi wa Bw Duale wakisema “wamekuwa wakifanya kazi katika hospitali mbali mbali nchini kwa zaidi ya miaka 10.” Walalamishi hao wameeleza katika kesi iliyowasilishwa na wakili Danstan Omari kwamba maagizo ya Bw Duale yanawabagua kwa vile wahudumu wengine katika sekta ya afya kutoka Uganda, Rwanda na mataifa ya Uingereza wanahudumu nchini. “Nchi ya DR Congo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tangu Aprili 2022 na tunatakiwa kufaidi kama wakazi wa Jumuiya hii. Agizo la Bw Duale la Januari 7, 2025 linatubagua. Twaomba Mahakama kuu ibatilishe agizo hili na kuturuhusu kupewa leseni na KMPDU,” Dkt Georges Maloba Banza aomba korti. Katika kesi iliyowasilishwa Dkt Banza, ambaye ni rais wa chama cha madaktari wa Congo wanaohudumu Kenya amedai agizo hilo la Bw Duale linakandamiza haki zao na ni kinyume cha Katiba ya Kenya ya 2010 inayosema kwamba wakazi wote wa Kenya wako na uhuru wa kufanya kazi ili kujikimu kimaisha. “Agizo la Bw Duale tunyimwe leseni ya kuhudumu nchini na pia vibali vya kufanya kazi nchini linabagua sisi,” asema Dkt Banza.