MAHAKAMA Kuu imepiga marufuku kwa muda mashirika ya umma na serikali za kaunti kuajiri mawakili binafsi pale ambapo kuna mawakili wa serikali au mawakili wa kaunti wanaoweza kushughulikia kazi husika. Uamuzi huo ulitolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na daktari wa upasuaji anayeishi Nakuru, Dkt Magare Gikenyi, pamoja na watu wengine sita, wanaodai kuwa kaunti na mashirika ya umma yanapoteza mamilioni ya pesa za walipa ushuru kila mwaka kwa kuajiri mawakili wa kibinafsi ilhali tayari wana mawakili wanaoweza kushughulikia kesi kama hizo. Wanasema hakuna msingi wa kikatiba unaoruhusu kuajiri mawakili wa nje huku walipa ushuru wakiendelea kulipia mishahara ya mawakili walioajiriwa na serikali. Mahakama ilithibitisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru nyaraka za taasisi zilizotajwa kwenye kesi hiyo ziundwe haraka upesi likiwemo Baraza la Magavana, Mwanasheria Mkuu, Tume ya Uchaguz (IEBC) na Tume ya Utumishi wa Umma. Katika uamuzi wake, mahakama ilitoa amri ya kusitisha kuajiri, kuendelea kuajiri au kulipa mawakili binafsi na kampuni za sheria na mashirika ya umma pale ambapo kuna mawakili waliopo, hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa. Aidha, Mdhibiti wa Bajeti, Dkt Margaret Nyakang’o, na watumishi wote wa umma waliagizwa kutoruhusu utoaji wa fedha zozote kwa huduma za kisheria za nje hadi kesi hiyo itakapokamilika. Uamuzi huo ulizua ukosoaji mkali kutoka kwa wanasheria. Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Bi Faith Odhiambo, alisema uamuzi huo utaathiri mawakili kifedha. Dkt Gikenyi alitaja mifano kadhaa, ikiwemo madai ya Sh243 milioni kulipwa kwa kampuni binafsi ya sheria katika mkataba wa Adani na ada za kisheria za IEBC za Sh445.5 milioni baada ya uchaguzi wa 2022, akisema matumizi hayo yanakiuka kanuni za matumizi ya busara ya fedha za umma. Kesi hiyo itatajwa tena Januari 30 kwa maelekezo zaidi.