RAIS William Ruto sasa analenga kuvutia kura za wanawake na vijana kupitia ahadi ya mabilioni ya fedha ambayo yamewekwa kwenye bajeti ya mwaka ujao. Hazina Kuu ya Fedha imeahidi kukumbatia miradi ya kuwainua vijana na wanawake katika mwaka wa kifedha wa 2026/27 kwa mujibu wa Stakabadhi ya Sera ya Bajeti ya 2026/27. Kwenye stakabadhi hiyo, serikali inalenga kusambaza Sh12 bilioni kwa makundi 16,850 ya wanawake na vijana pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 178,500 wanaotoka familia zisizojiweza kifedha. “Juhudi za kuhakikisha wasichana wapo shuleni zitapigwa jeki kwa wasichana milioni 11.1 kupewa taulo za hedhi. Pia manusura wa dhuluma za kijinsia watasaidiwa,” ikasema stakabadhi hiyo ya sera za bajeti. Serikali pia inalenga kusambaza Sh9.6 bilioni kwa wanawake 660,000 wanaofanya biashara. Pia kutakuwa na mafunzo ya kusaidia kutokomeza dhuluma za kijinsia na jinsi ya kutatua mizozo ya kinyumbani. Aidha, Hazina Kuu ya Fedha imeahidi kutenga Sh3.3 bilioni kwa makundi ya walemavu na wanawake, kuongeza pesa ambazo zinatumika kupiga jeki biashara za wanawake na pia kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo la Kupambana na Dhuluma za Kijinsia. Katika miaka ya kifedha ya 2022/23 na 2024/25 serikali ilisambaza Sh3.33 bilioni kwa makundi 10,785 ya wanawake na vijana na pia ikawalipia karo wanafunzi 155,580 kutoka familia maskini kupitia Hazina ya Serikali ya Kitaifa (NGAAF). Kupitia Hazina ya Wanawake (WEF), Sh3.12 bilioni zilisambaziwa wanawake 261,681 huku wanawake 361,481 wakipewa mafunzo kuhusu nidhamu katika matumizi ya fedha. Stakabadhi hiyo ya sera kuhusu matumizi ya pesa inaonyesha kuwa vijana 90,000 watapewa mafunzo ya kujiajiri na kutengeneza mali. Vijana wengine 43,000 watapata mafunzo kuhusu nafasi za kibiashara. [caption id="attachment_183308" align="alignnone" width="1280"] Rais William Ruto afurahia nyakati na vijana wakati wa kuzinduliwa kwa mradi wa Nyota, Nyeri. Picha|PCS[/caption] Katika tasnia ya sanaa, leseni 16,300 zitatolewa kwa watengenezaji filamu na pia kuwapa msaada wa kifedha wasanii wanaojipatia riziki kupitia muziki. “Serikali inalenga kuhakikisha vijana wengi wana ujuzi wa kufanya biashara, kujiajiri na kuwa nguzo ya ukuaji wa uchumi wa nchi,” ikasema stakabadhi hiyo. Mnamo 2025, Rais Ruto ameonekana anarejea kwa vijana na ahadi za ajira ambazo zilichochea wengi wamchague katika uchaguzi wa 2022. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki amekuwa akishiriki michango ya kuinua wahudumu wa bodaboda, mama mboga. Pia kumekuwa na mikutano mingi ikulu ambapo Rais amekutana na wasanii, viongozi wa kidini, vijana na makundi mengine yalimsaidia kutwaa mamlaka miaka minne iliyopita. Tangu waingie madarakani, utawala wa Kenya Kwanza umeanzisha miradi mbalimbali ambayo inalenga vijana. Kwa sasa, Rais Ruto anaonekana amechangamkia ule wa NYOTA ambapo anasambaza fedha kwa makundi ya vijana katika kaunti mbalimbali nchini. Hazina ya Hustler, kazi za mitandaoni, nafasi za mafunzo ya kazi ni kati ya miradi mingine aliyokumbatia kuwafaa vijana.