TEHRAN, IRAN MBUNGE wa Iran ameonya kuwa serikali itakabiliwa na maandamano makubwa zaidi iwapo haitashughulikia malalamishi ya wananchi huku maandamano ya kitaifa ya kupinga uhalali wa viongozi wa kidini nchini humo yakiendelea. “Tusisahau jambo moja: wananchi hawajaridhishwa na uongozi. La sivyo, matukio kama haya yatajirudia kwa nguvu zaidi,” alisema Mohammadreza Sabaghian, mbunge anayewakilisha kaunti kadhaa katika mkoa wa Yazd, katikati mwa Iran, alipokuwa akizungumza bungeni. Kauli hiyo imeongeza shinikizo kwa Tehran wakati mamlaka yakikabiliwa na mojawapo ya changamoto kubwa zaidi tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979. Rais wa Amerika, Donald Trump alitangaza Jumatatu usiku kuwa bidhaa zozote zinazoingizwa Washington kutoka nchi zitakazofanya biashara na Iran zitatozwa ushuru mpya wa asilimia 25. Hadi sasa, Tehran haijajibu rasmi tangazo hilo, lakini China, mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran, imepinga hatua hiyo ya Trump. Iran huuza sehemu kubwa ya mafuta yake kwa China, huku Uturuki, Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na India zikiwa miongoni mwa washirika wengine wakuu wa kibiashara. Mamlaka ya Iran ilisema Jumatatu kuwa bado inaweka wazi njia za mawasiliano na Washington, wakati Trump akitafakari hatua za kuchukua dhidi ya Iran. “Tuna wajibu wa kufanya mazungumzo, na bila shaka tutafanya hivyo,” alisema msemaji wa serikali Fatemeh Mohajerani, katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne. Mohajerani aliongeza kuwa Rais Masoud Pezeshkian ameagiza kuanzishwa kwa warsha ili kuchunguza sababu za hasira miongoni mwa vijana. Maandamano nchini Iran yalianza mnamo Desemba 28, 2025 wakati wafanyabiashara katika jengo la kibiashara la Grand Bazaar lililoko jijini Tehran walifunga maduka yao wakilalamikia kushuka kwa thamani ya sarafu wa Iran, Rial. Maandamano huyo yalienea haraka kote nchini humo huku malalamishi yakiwa kupanda kwa gharama ya maisha na utawala mbaya wa kidini nchini Iran. Iran imetawaliwa na viongozi wa kidini tangu Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanyika mnamo 1979. Kulingana na shirika la habari la kitaifa nchini Iran, jumla ya walinda usalama 109 wameuawa katika makabiliano na waandamanaji. Hata hivyo, hadi sasa, hakuna dalili za migawanyiko ndani ya uongozi wa kidini, jeshi au vikosi vya usalama. Waandamanaji pia hawana uongozi wa pamoja ulio wazi. Katika ujumbe alioutuma kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu usiku akitangaza ushuru huo mpya, Trump alisema: “Kuanzia sasa, nchi yoyote itakayofanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italipa ushuru wa asilimia 25.” Iran tayari iko chini ya vikwazo vizito vya Amerika, hali inayozidi kuathiri uchumi wake.