Uchunguzi waonyesha aliyefariki akikwea Mlima Kenya alikosa hewa

UCHUNGUZI wa maiti umebaini kuwa mwanamume aliyefariki akikwema Mlima Kenya, alifariki kutokana na kukosa hewa ya oksijeni, hatua iliyosaidia kuleta afueni kwa familia yake baada ya wiki kadhaa za sintofahamu. Samuel Macharia, ambaye alikuwa mwongoza watalii mwenye uzoefu mkubwa, alipotea Desemba 23 alipokuwa katika msafara wa kupanda Mlima Kenya. Mwili wake ulipatikana baadaye kufuatia operesheni kubwa ya utafutaji na uokoaji iliyohusisha taasisi mbalimbali. Upasuaji wa maiti ulifanywa Jumanne katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nanyuki na daktari wa serikali, mbele ya watU wa familia. Uchunguzi huo ulionyesha kuwa Macharia hakuwa na majeraha ya nje na viungo vyake vya ndani vilikuwa salama. Hata hivyo, ilibainika kuwa kukosa oksijeni ndiko kulikosababisha kifo chake. Msemaji wa familia, Lucy Kagwaine, alisema matokeo hayo yamepunguza maumivu ya familia baada ya siku nyingi za wasiwasi na maswali yasiyo na majibu kuhusu kutoweka kwake. “Uchunguzi wa maiti umefanyika na tumeridhika kama familia. Hakukuwa na majeraha yanayoonekana, na tumeelezwa kuwa alifariki kutokana na kukosa oksijeni mlimani,” alisema. Aliongeza kuwa ingawa majonzi bado yapo, matokeo hayo yamepatia familia amani ya moyo. Macharia alipotea akiwa na waongoza watalii wengine wanne waliokuwa wakisindikiza watalii wawili kutoka Japan waliokuwa wakijaribu kupanda mlima huo wa pili kwa urefu barani Afrika. Kulingana na Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS), mwili wake ulipatikana katika Bonde la Hinde, katika mwinuko wa takriban mita 4,300 kutoka usawa wa bahari. KWS ilisema mwili huo ulipatikana baada ya operesheni ya utafutaji iliyodumu muda mrefu na kuratibiwa vyema, ikihusisha walinzi wenye uzoefu, kikosi cha uokoaji milimani, uchunguzi wa anga na doria za ardhini. Maeneo yaliyotafutwa ni pamoja na Shipton Camp, Austrian Hut, Bonde la Mackinder, Sendeyo, Bonde la Hinde, Mintos, Njia ya Timau na maeneo jirani. Operesheni hiyo ilifanyika katika mazingira magumu yaliyojaa hali mbaya ya hewa, miinuko mikali na mwonekano hafifu.