Umaskini wasababisha zaidi ya wanafunzi laki 8 kukosa kuripoti shule

UMASKINI pamoja na hatua ya serikali kudhibiti uteuzi wa shule, umeibuka kuwa sababu kuu inayofanya zaidi ya wanafunzi 800,000 wa Gredi ya 10 kushindwa kuripoti katika shule walizoteuliwa. Katika Kaunti ya Murang’a, Jacinta Njiru, mama mlezi anayejipa riziki kama mama-fua mjini Maragua, anasema hata akipewa miaka 10 ya kuweka akiba, hawezi kumudu karo ya Sh55,000 kwa mwanawe aliyeteuliwa kujiunga na Shule ya Upili ya Njiiri. “Hiyo ni karo ya mwaka mmoja pekee. Pia ninatakiwa kununua mahitaji binafsi ya shule yanayozidi Sh25,000,” alisema. Njiru alisema mwanawe aliyefanya mtihani wa KJSEA katika Shule ya Msingi ya Kianjiru-ini hataripoti shuleni Njiiri, bali atabaki nyumbani hadi apate nafasi katika shule ya kutwa iliyo karibu. “Kumweleza mwanangu kuwa hatajiunga na shule aliyopata kwa juhudi zake ilikuwa kazi ngumu zaidi. Tulilia pamoja tulipotambua hali yetu ya umaskini, naye akanielewa akisema anajua hatuwezi kumudu elimu bora licha ya akili zake nyingi,” alisema. Alisema basari ya eneobunge la Maragua ilimsaidia kwa Sh5,000 pekee, kiasi ambacho hakitoshi kumpeleka mwanawe Njiiri. “Nina akiba ya Sh6,000 pekee. Bajeti yote ya mwaka mmoja ni Sh84,000. Katika ukoo wangu sijawahi kuona pesa za aina hiyo,” alisema. Kisa chake kinaakisi hali inayokumba familia nyingi katika eneo la Kati mwa Kenya, ambako hata taasisi za kifedha kama Family Bank, Equity, KCB na Cooperative zimekuwa kimya kuhusu udhamini wa wanafunzi kutoka familia maskini. Hali hiyo imezua wito kutoka kwa kampuni ya Rwathia Distributors, inayomilikiwa na matajiri wa Murang’a, waliotaka jamii ya Mlima Kenya kuchukulia kushindwa kwa watoto kujiunga na shule za sekondari kama janga la kikanda. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Kanene Kabiru, alisema: “Ni wakati mwafaka kwa sisi wenyewe kuchukua hatua kama jamii. Tuwatafute watoto hawa na kuwasaidia binafsi. Hili sasa ni janga la kijamii.” Katika Kaunti ya Meru, shule kadhaa ziliripoti idadi ndogo ya wanafunzi siku ya kwanza na ya pili ya kuripoti. Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Meru, Joseph Maki, alisema hali hiyo ilishuhudiwa katika eneo zima, huku shule za ngazi ya chini zikiathirika zaidi. “Kuanzia kwa wanafunzi wa shule za kitaifa kumekuwa idadi ya wanaoripoti imekuwa ya chini sana. Shule zinazotarajia wanafunzi 100 zimepokea takriban 10 pekee. Tunatumai hali itabadilika kufikia Ijumaa,” alisema. Katika Shule ya Meru, mojawapo ya shule za kitaifa, wanafunzi 450 pekee kati ya 720 waliripoti siku ya kwanza. Mkuu wa masomo wa shule hiyo, Mark Namaswa, alihusisha hali hiyo na changamoto za kifedha kutokana na muda wa kuripoti. “Kihistoria, wanafunzi wa kidato cha kwanza waliripoti mwishoni mwa Januari, jambo lililowapa wazazi muda wa kujiandaa kifedha. Kuripoti mara tu baada ya likizo kumeathiri wengi,” alisema. Mkuu wa Shule ya Upili ya Nkubu, Henry Imunya, alisema idadi ya wanafunzi walioripoti ilikuwa ndogo ikilinganishwa na miaka iliyopita. “Idadi ya wanafunzi kulingana na orodha ya wizara inatia wasiwasi. Changamoto zinatokana na matatizo ya awali ya mfumo mpya wa uteuzi mtandaoni na umaskini uliokithiri kufuatia mvua kukosa,” alisema. Aliongeza kuwa mipango mbalimbali ya ufadhili pia haipo mwaka huu. Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Kirigara, Agnes Mwiti, alisema wamepokea zaidi ya wanafunzi 300 dhidi ya uwezo wa 600. Katika Kaunti za Kirinyaga na Embu, wanafunzi wengi hawajaripoti baada ya kuteuliwa shule zilizo mbali na kaunti zao, huku wazazi wakishindwa kumudu nauli kubwa ya usafiri. “Baadhi ya watoto wetu wameteuliwa shule ambazo hawakuchaguam Magharibi na Nyanza, na nauli ni kubwa mno,” alisema mzazi mmoja. Wengine bado wako nyumbani kwa sababu ya umaskini. “Mwanangu aliteuliwa kujiunga na Shule ya Upili ya Kianyaga baada ya kupata alama 66 katika KJSEA, lakini alishindwa kujiunga kutokana na kukosa karo,” alisema Anthony Njogu kutoka Kirinyaga. Alieleza hofu kuwa mwanawe huenda akabaki nyumbani iwapo hatapata mfadhili wa kumwezesha kujiunga na shule ambayo amekuwa akitamani. Katika kaunti za Kilifi, Lamu, Nyamira, Kisii, Homa Bay na Kisumu, wazazi wengi walisema umaskini na hali ngumu ya kiuchumi imewalazimu kuwaacha watoto nyumbani licha ya kupata nafasi katika shule za kitaifa na zile za nje ya kaunti. Baadhi ya wanafunzi pia wanatafuta uhamisho baada ya kupelekwa shule zilizo mbali na nyumbani au zisizoendana na matarajio yao ya taaluma. Wakuu wa shule wanasema idadi ndogo ya wanafunzi walioripoti inafanya iwe vigumu kuanza rasmi masomo. Kwa mfano, baadhi ya shule zimeripoti kupokea chini ya wanafunzi 50 kati ya zaidi ya 500 waliotarajiwa. Hali hii imeleta msongo wa mawazo kwa wanafunzi na wazazi, huku baadhi ya watoto wakipatwa na huzuni kubwa kwa kushindwa kujiunga na shule walizoota. Wadau sasa wanaitaka serikali kuongeza muda wa kuripoti, kuharakisha utoaji wa bursary na kuweka mikakati mahsusi ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayebaki nyuma kwa sababu ya umaskini.