‘Sultani’ Joho asipokuwa mezani katika dili ya ODM-UDA heri ikae, viongozi Pwani waonya

MDAHALO unaotarajiwa kati ya chama cha ODM na UDA kuhusu muungano wa 2027, umeibua msisimko mpya katika eneo la Pwani, ambapo wanasiasa wanasisitiza Waziri wa Madini, Bw Hassan Joho, awakilishe eneo hilo katika mazungumzo hayo. Chini ya Kikundi cha Wabunge wa Pwani (CPG), viongozi hao kutoka vyama tofauti walisema eneo hilo limekuwa nguzo kuu ya chama hicho kwa muda mrefu, na hawatakubali kutengwa kwenye meza ya kujadili siasa na maendeleo. "Tunataka Pwani iwakilishwe kwenye meza za mazungumzo. Hatubembelezi. Tumeanza mwaka tukiwa na umoja bila kujali tofauti zetu za kisiasa," alisema Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kilifi, Bi Getrude Mbeyu, huku akidai kutwaa nafasi ya uenyekiti katika CPG. Bi Mbeyu alizungumza baada ya mkutano wa faraghani uliohaudhuriwa pia na Bw Joho jijini Mombasa. Hata hivyo, wanasiasa wanaounga mkono upinzani unaoongozwa na Kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, na aliyekuwa naibu rais, Bw Rigathi Gachagua, hawakuhudhuria mkutano huo. Hivi majuzi, wanasiasa wa Pwani wanaoegemea upande wa Rais William Ruto, walitaka Bw Joho apewe wadhifa wa kiongozi wa ODM. Hatua hii ilionekana kulenga kumweka katika nafasi bora ya kuongoza mazungumzo yoyote ya muungano, na vilevile kumweka pazuri kupewa wadhifa mkubwa endapo muungano wao utashinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.