Ni kilio, hasara jijini biashara, makazi yakiharibiwa kupisha miradi ya serikali

MPANGO wa serikali wa kutekeleza miradi ya mabilioni ya pesa umesababisha kilio, hasara na mahangaiko kwa walalahai na walalahoi, kutokana na uharibifu wa mali unaotokea kupitia ubomozi wa makazi na maeneo ya kibiashara. Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi ameonja shubiri hiyo baada ya biashara yake ya mamilioni ya pesa kuangushwa karibu na uwanja wa Nyayo kando ya barabara ya Douglas Wakihuri mnamo Jumanne usiku. Bw Wamatangi na wafanyabiashara wengine walikuwa wakiendesha biashara ya kuosha magari, hoteli, urembo na maduka ya kuuza vileo eneo hilo. Tukio hilo linakuja baada ya wakazi wa mtaa wa Makongeni eneobunge la Makadara, Nairobi kuangushiwa nyumba na kufukuzwa mtaani humo mnamo Desemba kwenye ubomozi ambao haukusaza makanisa na vibanda vya kibiashara. Serikali ilibomoa makazi katika Mtaa wa Makongeni, ikisema hatua hiyo itapisha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu huku wakazi wengi wakihangaika na kukosa pa kuenda. Kwenye mtaa wa South B, zaidi ya familia 5,000 walihamishwa kwa lazima wiki hii serikali ikilenga kuendeleza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu mtaani humo. Wakazi walisimulia jinsi walivyotishwa na wuhuni huku baadhi wakipokea Sh30,000 ambazo serikali ilikuwa ikiwapa ndipo wahame lakini wakidai ni kidogo ikilinganishwa na hasara waliyopata. Jana, walioshuhudia biashara za Bw Wamatangi zikiangushwa, walisema maafisa wa usalama walifukuza kila mtu na kurusha vitoza machozi kuzuia upinzani wowote. Festus Inyambuko ambaye alikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya kusafisha mkeka ya Supershine inayomilikiwa na gavana, alisema polisi waliwasili saa mbili usiku pamoja na matingatinga ya kuangusha majengo. “Tulijaribu kadri ya uwezo wetu kwa sababu tulikuwa na amri ya korti. Kwa muda mwingi usiku tulifaulu kudhibiti hali,” akasema Bw Inyambuko. Hata hivyo, maji yalizidi unga kati ya saa nane na saa tisa usiku, wakati polisi zaidi waliwasili. “Tulimwona Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen akiwasili hapa kwenye gari lake na akaamrisha polisi zaidi waje kutoa ulinzi ubomozi ukiendelea,” akasema Bw Inyambukho. “Walituzidi nguvu na wakati huo hata baadhi ya mali ikaporwa. Tumepoteza mali na pahala pa kupata riziki. Inashangaza serikali inasema inabuni nafasi za ajira ilhali sasa hapa hatuna kazi,” akasema Maxwel Yago, mfanyakazi mwingine katika majengo hayo. Hasara iliyotokea ilikuwa dhahiri pale majengo yaliyoangushwa na mali ndani yakiporomokea yakiwemo magari ya kifahari yaliyokuwa yameegeshwa. Mchanga ulifunika magari hayo huku wafanyabiashara na wahudumu kwenye biashara hizo, baadhi wakiwa wameweka mikono kichwani wakikadiria hasara na kudondokwa na machozi. Kabla ya Gavana Wamatangi kuwasili, kundi la viongozi wa kidini wa madhehebu mbalimbali kwa kufahamu hasara iliyotokea, walifika wakaomba na kuongea kwa ndimi wakilaani tukio hilo. Huzuni ilikuwa dhahiri usoni mwa Bw Wamatangi ambaye aliwasili akiwa amevalia suti ya samawati huku akitazama na kuangalia jinsi mali aliyokuwa akijivunia, ilikuwa imefunikwa na mchanga. Gavana huyo alizunguka eneo hilo, akionekana mwenye fikira nyingi huku akitembea na kutozungumza sana. Alipowahutubia wanahabari, alisema analengwa kisiasa na kuna baadhi ya viongozi wanaomtaka anyamaze na kutozungumzia siasa za nchi. “Koma kutumia afisi za serikali kunizamisha. Koma kuwatumia maafisa wa serikali kuharibu mali yangu na kunihangaisha. Hili ni tukio la uoga,” akasema Bw Wamatangi alipowahutubia wanahabari eneo hilo. Alisema kuangushwa kwa mali yake kulitokea baada ya vitisho dhidi yake siku chache zilizopita. “Wamekuwa wakinionya kwamba wanakuja siku tano zilizopita na kuwa nikae ange. Niliwaambia waliokodisha nyumba zangu hapa wawe macho na kwa masikitiko makuu polisi walikuja jana usiku na kuharibu mali,” akaongeza. Kinaya ni kwamba ubomozi wenyewe uliendelezwa licha ya amri ya korti ya kuuzuia kutolewa mnamo Jumanne. Shirika la Reli nchini linadai ardhi kulikojengwa biashara na mali ya Bw Wamatangi ni yake na inalenga kujenga reli ya kufika hadi uwanja wa Talanta ambao ujenzi wake unaendelezwa na serikali. Hata hivyo, kiongozi huyo anasema alikodisha ardhi hiyo kwa kipindi cha miaka 65 na amekuwa akilipa ada kwa kuyazingatia maelewano yao bila kufeli. “Mimi ni mtu wa maendeleo na si siasa na ubomozi huu unalenga kuniondoa kama kiongozi ambaye si mchapakazi ili niwe kama wanasiasa wengine,” akasema gavana huyo. Licha ya amri ya korti kuwepo, KR ilitetea ubomozi huo, ikisema nyuga tatu za Nyayo, MISC Kasarani na Talanta lazima ziunganishwe kwa uchukuzi wa reli kwenye Kombe la Afrika (AFCON) mwaka ujao. “Waliojenga kwenye ardhi ya KR walishauriwa na hata kupewa notisi ya kuondoka na hata wakaambiwa vibanda vyao vingeondolewa wakikosa kufanya hivyo,” ikasema taarifa ya KR ingawa hawakueleza kwa nini waliendelea na ubomozi licha ya uwepo wa amri ya korti. Katika mtaa wa Mariguini, Mary Mbone ambaye ameishi eneo hilo kwa miaka 30 ni kati ya wakazi ambao wanasema hawana mahala pa kuenda baada ya nyumba aliyojenga kubomolewa. Wakazi wamekuwa wakililia serikali angalau itekeleze ubomozi kwa heshima na kuwaarifu ili kuzuia uharibifu wa mali.