WADAU katika sekta ya mawasiliano wameibua wasiwasi kuhusu mfumo wa bei uliotumika katika pendekezo la kuuzwa kwa asilimia 15 ya hisa za serikali katika kampuni ya Safaricom Limited, wakionya kuwa bei ya Sh34 kwa kila hisa huenda ikawa ya chini kuliko thamani halisi. Wataalamu hao pia wameonya kuwa ikiwa kampuni ya Vodacom ya Afrika Kusini itamiliki hisa nyingi katika Safaricom kuna hatari ya kupunguza ushawishi wa serikali katika maamuzi muhimu ya kimkakati. Taasisi ya Wahasibu Kenya (ICPAK) na Chama cha Watoa Huduma za Teknolojia Kenya zilisema kuwa katika uuzaji huo wa Safaricom, bei ya Sh34 kwa kila hisa iliwekwa bila kuwepo kwa maelezo ya wazi kuhusu mbinu ya tathmini iliyotumika. “Bei iliyopendekezwa ya Sh34 kwa kila hisa haijaambatana na maelezo ya wazi ya mbinu ya tathmini, hali inayozua maswali kuhusu uwazi na uwajibikaji,” alisema Prof Elizabeth Kalunda, mwenyekiti wa ICPAK. Haya yanajiri huku Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA), Mamlaka ya Mawasiliano (CA) na Mamlaka ya Ushindani (CAK) zikiunga mkono uamuzi wa kuuza sehemu ya hisa za serikali, zikisema bei hiyo haitakuwa na athari hasi kwa soko. Serikali inalenga kukusanya takribani Sh204 bilioni kupitia uuzaji wa hisa milioni sita kwa Vodacom kwa bei ya Sh34 kila moja. Kwa sasa, serikali inamiliki asilimia 35 ya Safaricom. Baadhi ya wabunge wameeleza hofu kuhusu usalama wa kitaifa na umiliki wa data iwapo Vodacom itapata umiliki wa asilimia 55. Wadau wameitaka serikali kuweka ulinzi mahsusi, ikiwemo uwazi kamili wa tathmini, kulinda maslahi ya taifa, wafanyabiashara na uthabiti wa kiuchumi kabla ya kuendelea na ubinafsishaji huo.