MAONI: Ni uzembe na kejeli kuiga Truphena kukumbatia mti

BAHATI ya mwenzio usiilalie mlango wazi,’ ni msemo ambao haujawahi kudhihirika kwa njia bora zaidi kuliko ilivyokuwa katika majuma machache yaliyopita. Mnamo Desemba 8, mwaka jana, Truphena Muthoni, 22, alijitokeza hadharani kwa jaribio la aina yake la kukumbatia mti kwa saa 72. Hatua hiyo iliashiria “kulalamikia kimyakimya” ukataji miti kiholela, kubadilisha matumizi ya ardhi ya misitu na kukosa kulinda kikamilifu chemichemi za maji na kuitisha uwajibikaji kutoka kwa umma na viongozi. Haikuwa mara ya kwanza kwa binti huyu ambaye ni mtetezi sugu wa uhifadhi wa mazingira ambaye alivikwa taji la rekodi ya kukumbatia mti kwa muda mrefu zaidi wa saa 48, kati ya Januari 31 – Februari, 2025. Katika rekodi hiyo iliyotambuliwa na shirika la kimataifa la kuhifadhi matukio ya kipekee, Guinnes World of Records, Truphena alikusudia kuhamasisha manufaa ya kukumbatia mti kwa afya ya kiakili na hisia. Baada ya kustahimili hali ya anga iliyobadilikabadilika karibu na afisi za serikali ya kaunti ya Nyeri akiwa amekumbatia mti kwa siku tatu bila kulala, kula wala kunywa, binti huyu alivunja rekodi yake mwenyewe ya saa 48! Ufanisi wa Truphena ulisherehekewa kote nchini na kuvutia tuzo kochokocho ikiwemo Sh1 milioni, hati ya kumiliki ardhi, simu aina ya Samsung Fold 7, ziara kwenda Dubai na kukutana na Rais William Ruto kati ya mengineyo. Hata hivyo, ufanisi wake haukuwa rahisi. Kando na kustahimili dhihaka mitandaoni, Truphena aliandaa mwili wake kwa miezi mitano kwa mazoezi makali. Kwa kufuatilia kwa makini safari ya Truphena, ni bayana kuwa ni binti mwenye ari na ushupavu wa kufuata ndoto yake pasipo kujali dhihaka wala vikwazo vyovyote. Inashangaza hivyo basi, kuona watu kadhaa, wake kwa waume, wakijitokeza kukumbatia miti siku chache tu baada ya ufanisi wa Truphena. Kenya inashuhudia ‘mlipuko wa kukumbatia miti’ ambapo baadhi ya watu wameishia kulazwa hospitalini baada ya kuathirika kiafya na kuzimia wakijaribu “kumwiga” mwanadada huyo. Japo maazimio yao yanastahiki kabisa kuanzia uhamasisho kuhusu saratani, kuchangisha hela za karo hadi kuwataka viongozi kuwajibika na kuhimiza amani kabla ya uchaguzi mkuu 2027, wanaojaribu kumwiga Truphena wanakosa mshawasha na uasilia. Hali kwamba tunashuhudia matukio haya muda mfupi tu baada ya Truphena kutamba nchini na kimataifa kwa kukumbatia mti inawasawiri wanaomwiga kama wasio wabunifu na wanaomezea mate nyota na bahati yake.