WHO yashinikiza ushuru mkali kwa bidhaa za sukari na pombe

Shirika la Afya Duniani (WHO) linataka serikali kote ulimwenguni kuimarisha kwa kiasi kikubwa ushuru kwa vinywaji vyenye sukari na vileo, likionya kuwa mifumo dhaifu ya kodi inahujumu juhudi za kulinda afya ya umma na kuacha mifumo ya afya ikibebeshwa mzigo mkubwa. Kwa mujibu wa WHO, vinywaji vyenye sukari na vileo vinazidi kuwa nafuu kutokana na viwango vya chini vya ushuru katika nchi nyingi. Mwelekeo huu unasababisha kuongezeka kwa unene kupita kiasi, kisukari, magonjwa ya moyo, saratani na majeraha, hasa miongoni mwa watoto na vijana. Wito huo ulitolewa wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti mbili mpya za kimataifa: Ripoti ya Kimataifa kuhusu Matumizi ya Ushuru wa Pombe, 2025, na Ripoti ya Kimataifa kuhusu Matumizi ya Ushuru wa Vinywaji Vilivyoongezwa Sukari, 2025. Ripoti hizo zinaonya kuwa ushuru hafifu unaruhusu bidhaa hatari kuwa za bei nafuu huku serikali zikikosa fedha za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na majeraha yanayoweza kuzuilika. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema kuongeza ushuru kwa bidhaa hatari kwa afya kama tumbaku, vinywaji vyenye sukari na pombe kunaweza kupunguza matumizi mabaya huku kukizalisha mapato kwa huduma muhimu za afya. “Ushuru kukinga afya ni mojawapo ya nyenzo madhubuti zaidi tulizo nazo za kukuza afya na kuzuia magonjwa,” alisema Dkt Tedros. WHO ilibainisha kuwa soko la kimataifa la vinywaji vyenye sukari na vileo huzalisha faida ya mabilioni ya pesa, lakini serikali hupata sehemu ndogo sana ya mapato hayo kupitia ushuru, na kuziacha jamii kubeba gharama za muda mrefu za afya na uchumi. Ripoti zinaonyesha kuwa angalau nchi 116 kwa sasa zinatoza ushuru vinywaji vyenye sukari, hasa soda. Hata hivyo, bidhaa nyingi zenye sukari nyingi kama juisi asilia za asilimia 100, vinywaji vya maziwa vilivyotiwa sukari, na kahawa au chai tayari kwa kunywa bado hazitozwi ushuru kwa kiasi kikubwa. Ingawa asilimia 97 ya nchi zinatoza ushuru vinywaji vya kuongeza nguvu, WHO ilisema kiwango hicho hakijabadilika tangu ripoti ya mwisho ya 2023, ikionyesha maendeleo ya polepole. Katika bajeti ya Kenya ya 2025, serikali ilianzisha Ushuru wa Maendeleo ya Sukari (SDL) wa asilimia nne kwa sukari yote, ya kuagizwa na ya ndani, kuanzia Julai mwaka jana. Ingawa ushuru huo ulilenga kusaidia sekta ya sukari, ulisababisha pia kupanda kwa bei ya sukari.