RAIA wawili wa Uturuki wamezuiliwa rumande kwa wiki mbili, wakichunguzwa kwa madai ya ugaidi baada ya kuhusika katika mzozo barabarani na wanasiasa wa chama cha ODM mnamo Jumatatu. Mzozo huo ulitokea wanasiasa hao walipokuwa wakitoka kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi uliofanyika Kilifi. Wawili hao, mfanyabiashara Osman Erdinc Elsek na mwenzake Gokmen Sandikci, walifikishwa katika Mahakama ya Mombasa mnamo Jumatano, ambapo upande wa mashtaka ulisema wanashukiwa kuhusika na ufadhili wa shughuli za kigaidi. Katika hati ya mahakama iliyonakiliwa na afisa wa Kitengo cha Polisi wa Kupambana na Ugaidi (ATPU), Bw Bw Hassan Sugal, ilisemekana Bw Sandikci hakuwa na kitambulisho chochote wakati wa kukamatwa, huku Bw Elsek akipatikana akiwa na cheti cha mkimbizi cha Kenya. Walikamatwa katika eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, na baadaye kupelekwa Kituo cha Polisi cha Nyali, ambako walizuiliwa. Wapelelezi waliongeza kuwa Bw Sandikci alikuwa amebeba bunduki aina ya Glock, iliyojaa risasi 15. “Silaha hiyo na risasi zilichukuliwa na kuzuiliwa na DCI Nyali,” Bw Sugal alieleza. Mbali na ufadhili wa ugaidi, polisi walisema wawili hao pia wanachunguzwa kwa matumizi mabaya ya silaha kinyume cha Sheria ya Silaha. “Kabla ya kukamatwa, Kitengo cha ATPU Pwani kilipokea taarifa za kuaminika kwamba washtakiwa walihusishwa na ufadhili wa ugaidi ndani ya nchi. Kitengo hicho kilikuwa tayari kikiwa katika ufuatiliaji wa washukiwa kabla ya kukamatwa kwao,” Bw Sugal aliongeza. Vilevile, polisi walisema uchunguzi zaidi unahitajika, ikiwa ni pamoja na kuchunguza rekodi za washukiwa za kifedha na benki, rekodi za simu, vitambulisho na iwapo ni wakimbizi. Polisi pia waliambia mahakama wanahitaji muda kubaini makazi ya washukiwa ili kufanya ukaguzi wa mali, nyaraka au vifaa vinavyohusiana na uchunguzi unaoendelea. Walieleza hofu kwamba washukiwa wanaweza kutoroka wakiachiliwa huru, wakidai makazi yao bado hayajulikani. Kwa msingi huo, waliomba amri ya kuwazuilia wawili hao kwa siku 15 katika Kituo cha Polisi cha ATPU Mombasa ili kuruhusu uchunguzi kuendelea. Hata hivyo, Bw Elsek alipinga madai hayo, akisisitiza kwamba kesi hiyo ilitokana na ajali ya barabarani na mzozo wa kisiasa, wala si shughuli yoyote ya ugaidi. Bw Elsek alisema kuwa siku ya tukio, alikuwa akiendesha gari lake kisheria katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi, kutoka eneo la Vipingo kuelekea Kikambala. “Nilipofika Majengo, Kanamai, gari lilikuja kutoka nyuma kwa kasi, likapita kiholela na kugonga gari langu bila kusimama,” alisema. Aliongeza kuwa, magari matatu zaidi yalimpita kwa kasi, jambo lililosababisha aanze kuwafuatilia. “Mwishowe nililazimisha gari lililogonga gari langu lisimame kwa sababu nilihitaji maelezo kuhusu kuendesha kiholela, mgongano na uamuzi wa kutoroka,” Bw Elsek alisema. Kulingana na hati yake ya maelezo, watu wawili walishuka kutoka katika gari hilo na kuanza kugombana. “Walijaribu kunipiga kwa kutumia silaha, na nilipigwa na kujeruhiwa katika mchakato huo,” alisema. Bw Elsek alisema baadaye alitambua kwamba mmoja wa waliokuwa katika gari lililomgonga alikuwa Gavana wa Wajir, Bw Ahmed Abdullahi, na kwamba magari manne mengine yaliyokuwepo yalikuwa sehemu ya msafara wa gavana huyo. Bw Elsek pia alipinga madai kwamba alikuwa mwenye hatari ya kutoroka au kwamba makazi yake hayajulikani. Mahakama iliruhusu polisi kuwazuilia kwa wiki mbili huku uchunguzi ukiendelea.