KAMPALA, UGANDA RAIA wa Uganda wanasubiri kumfahamu rais na wabunge wao wapya baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika jana. Mshindi wa urais atatangazwa baadaye leo au kesho iwapo shughuli za kuhesabu kura zitakamilika upesi. Katiba ya Uganda inaamrisha matokeo ya mshindi wa urais lazima yatangazwe saa 48 baada ya kura kupigwa. Idadi ndogo ya wapigakura milioni 21.6 walijitokeza kushiriki kura hizo ambapo Rais Yoweri Museveni anasaka kuendeleza uongozi wake ulioanza mnamo 1986 kupitia chama cha NRM. Mwanasiasa Msanii Robert Kyangulanyi maarufu kama Bobi Wine anagombea urais kupitia chama cha upinzani NUP. Serikali iliagiza intaneti izimwe mnamo Jumanne kama sehemu ya kuzuia kusambazwa kwa jumbe za uchochezi na chuki. Jijini Kampala na maeneo mengine watu wachache waliojitokeza walikosa kupiga kura kwa wakati baada ya kufeli kwa mitambao ya kuwatambua wapigakura. Baadhi yao waliamua kurudi nyumbani huku wengine wakisubiri na kusababisha milolongo mirefu ionekane. Akipiga kura yake kituo cha upigaji kura cha Kasangati, mkazi Ronald Tenywa, ambaye ni Mhadhiri wa chuo kikuu alilalamika kuwa viongozi wa kisiasa hupambana kukwamilia mamlakani katika kila uchaguzi. “Tukipiga kura kwa mtu anayejali basi maisha yatakuwa mazuri sana kwa raia wa Uganda. Kuna viongozi ambao hukwamilia mamlaka na hawafanyi chochote,” akasema Tenywa, kauli iliyofasiriwa kumlenga Museveni. Huku mitambo ya kuwatambua wapigakura kupitia mfumo wa kielektroniki ikifeli, baadhi walizua maswali jinsi serikali ilitaka mitambo hiyo ifanye kazi bila intaneti. Mnamo Jumanne Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda Simon Byabakama alidai kuwa ametishiwa na baadhi ya maafisa wa serikali dhidi ya kumtangaza mgombeaji fulani kama rais. “Sitatishwa kwa sababu siko katika biashara ya kupeana kura. Baadhi ya watu wanasema usipomtangaza fulani kama rais, utakiona,” akasema. “Kile ambacho wapigakura watakisema ndicho nitakitangazia taifa. Ni wao ndio wanaamua rais ni nani,” akaongeza. Museveni na Wine bado hawakuwa wamepiga kura kufikia saa nane mchana.