POLISI katika Kaunti ya Nandi wamemulikwa baada ya madai ya kuwashambulia kikatili vijana waliokuwa wakicheza pool Nandi Hills, huku uchunguzi rasmi ukianzishwa kufuatia kisa hicho kilichozua ghadhabu miongoni mwa wananchi. Katika video iliyosambazwa mitandaoni, maafisa wapatao 10 wa polisi waliovalia sare, wakiwa wamejihami kwa bunduki na marungu, wanaonekana wakivamia ukumbi wa pool saa tano na dakika hamsini na moja usiku na kuwaamuru vijana waliokuwamo kulala chini kabla ya kuwapiga vikali. Kanda za CCTV zinaonyesha polisi hao wakitumia marungu na vijiti vya pool kuwacharaza vijana hao, huku vilio vyao wahurumiwe vikipuuzwa. Vijana hao waliamriwa kutoa vitambulisho vyao vya kitaifa na kueleza kwa nini walikuwa wakicheza pool usiku wa manane, huku maafisa wakipokezana zamu kuwapiga kwa takriban dakika 10. “Lala chini na uume kitambulisho chako cha taifa,” mmoja wa maafisa anasikika akisema katika video hiyo iliyorekodiwa Januari 10, 2026. Baada ya maafisa hao kuondoka, vijana walibaki ndani ya ukumbi wakiwa na hofu, wakishindwa kuamua iwapo watoke au wabaki kwa kuogopa kushambuliwa tena. “Tufanye nini sasa? Huenda wako nje wakitusubiri watupige tena,” mmoja wao anasikika akisema. Vijana waliodhulumiwa walisema walipigwa kikatili licha ya kutii maagizo yote waliyopewa, na sasa wanalenga kushtaki maafisa hao. Philip Letting alisema alijiunga na wenzake kucheza pool baada ya kufunga biashara yake kama njia ya kupumzika, lakini polisi waliwavamia na kuwashambulia bila sababu, akapata majeraha mikononi na mgongoni. Jumla ya vijana 15 walipata matibabu katika vituo mbalimbali vya afya, huku baadhi yao wakipata fomu za P3 kufuatilia haki yao mahakamani. Geoffrey Korir alisema haelewi kwa nini polisi walitumia nguvu kupita kiasi ilhali walikuwa wamejisalimisha na hawakufanya kosa lolote. Wengine walitaja tukio hilo kuwa ukiukaji wa haki za binadamu na kudai hatua kali zichukuliwe dhidi ya maafisa waliohusika. Victor Kiprono Kogo alisema sheria inapaswa kuchukua mkondo wake kwa haraka dhidi ya maafisa wanaotumia vibaya mamlaka yao. Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) jana ilisema imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo la Januari 10, huku baadhi ya waathiriwa na mashahidi tayari wakiwasiliana na mamlaka hiyo baada ya maafisa kutumwa Nandi. Mwenyekiti wa IPOA, Ahmed Issack Hassan, alisema mamlaka hiyo inalaani matumizi ya nguvu zisizo za lazima na kuwataka wananchi kuwa watulivu uchunguzi ukiendelea. Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, pia aliamuru Kitengo cha Masuala ya Ndani kuchunguza suala hilo. Wakati huo huo, kamati ya usalama ya kaunti ilifanya kikao cha dharura kufuatia ghadhabu ya umma kuhusu kile kilichotajwa kuwa matumizi kikatili ya nguvu na maafisa wa usalama. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nandi, Samuel Muukusi, alisema uchunguzi unaendelea na akaahidi kutoa taarifa kamili baadaye. Viongozi mbalimbali wamelaani tukio hilo na kutaka maafisa waliohusika wakamatwe na kushtakiwa. Gavana wa Nandi, Stephen Sang, alitaja shambulio hilo kuwa kinyume cha sheria na lisilokubalika, huku Seneta Samson Cherargei akimtaka Inspekta Jenerali kuwasimamisha kazi mara moja maafisa hao ili kuruhusu uchunguzi huru. Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, pia alitaka maafisa hao wakamatwe na kushtakiwa, akisema kucheza pool si kosa la jinai na kwamba raia hawalazimiki kubeba vitambulisho vyao kila wakati.