CHAMA cha Wanasheria nchini (LSK) kinataka Bunge kukataa pendekezo la serikali la kuuza asilimia 15 ya hisa zake katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, kikisema mchakato huo umeharakishwa, hauko wazi na haujafuata ushindani unaohitajika kisheria. LSK iliwasilisha hoja hiyo mbele ya kamati ya pamoja ya Bunge la Kitaifa ya Fedha na Mipango ya Kitaifa pamoja na ile ya Deni la Umma na Ubinafsishaji, ikitaka wabunge wakatae kuidhinisha mpango huo kwa sasa hadi tathmini ya thamani ya hisa hizo ifanywe kwa uwazi na kuthibitishwa na taasisi huru, pamoja na kuwekwa kwa muundo wazi na shindani wa uuzaji kwa mujibu wa Kifungu cha 201 cha Katiba. Wizara ya Fedha tayari imetia saini mkataba wa kuuza asilimia 15 ya hisa za Safaricom kwa kampuni ya Vodacom Group ya Afrika Kusini kwa bei ya Sh34 kwa kila hisa, hatua itakayoingizia serikali jumla ya Sh204.3 bilioni. Makamu wa Rais wa LSK, Mwaura Kabata, alisema uuzaji wowote wa mali ya umma unapaswa kuungwa mkono na mbinu za wazi za kutathmini thamani, tathmini ya muda mwafaka wa uuzaji kulingana na hali ya soko, na mfumo wa wazi wa kifedha unaoonyesha kuwa mapato yatatumika kupunguza deni la taifa au kuwekeza katika miradi ya uzalishaji, badala ya kuziba mapengo ya bajeti ya muda mfupi. LSK ilionya kuwa uuzaji huo utasababisha umiliki wa kigeni katika Safaricom kufikia asilimia 55, hali itakayofanya serikali kuwa mwenye hisa mdogo huku Vodacom ikidhibiti kampuni hiyo. Kwa sasa, Vodacom inamiliki asilimia 35 ya hisa za Safaricom, na ikikamilisha ununuzi wa asilimia 15 kutoka kwa serikali pamoja na asilimia tano nyingine kutoka kampuni mama ya Vodafone Group, itapata udhibiti kamili wa kampuni hiyo. Umiliki wa serikali, kwa mujibu wa mpango huo, utashuka hadi asilimia 20. “Hili linahatarisha uwezo wa kimkakati wa Kenya kudhibiti miundombinu ya kitaifa ya data, mifumo ya pesa za simu na sera za ushindani, huku sekta nyeti za kifedha na kiusalama zikiwekwa katika ushawishi wa kigeni,” alisema Bw Kabata.