Furaha mwanafunzi wa mama asiyeona akijiunga na Sekondari Pevu

WIKI jana, Teddy Kahindi mwenye umri wa miaka 18 aliingia katika Shule ya Upili ya Shimo La Tewa akiwa amevaa nguo zilizochanika na viatu vya plastiki, akiongozwa na mamake asiyeona, Bi Stella Kadzo. Leo, taswira hiyo ya kukata tamaa imegeuka kuwa simulizi ya matumaini makubwa. Baada ya habari ya Bi Kadzo—aliyeishi miaka mingi akiombaomba mitaani Malindi ili kuwasomesha na kuwalisha watoto wake—kuchapishwa Taifa Dijitali na kusambaa kwa kasi mitandaoni, Wakenya kutoka matabaka mbalimbali walijitolea kusaidia. Kufikia Ijumaa, jumla ya Sh53,544 zilizohitajika kusajili Teddy shuleni zilikuwa zimepatikana, pamoja na fedha za sare, malazi, na zana za sanaa. Kampuni ya Mombasa Cement Limited ililipa karo ya mwaka mzima. Mnamo Ijumaa asubuhi, Teddy alitoka mitaani na kuingia darasani rasmi. Shule ililipuka kwa shamrashamra alipofika, wakati huu akiwa amebeba sanduku jipya la chuma badala ya kushika mkono wa mamake pekee. Akiwa amevalia shati jeupe na suruali ya kijivu ya Shimo La Tewa, msanii huyo chipukizi alishindwa kuficha tabasamu lake. Alishuka kutoka gari la Katibu wa Wizara ya Vijana na Michezo, Jacob Fikirini, aina ya Toyota Land Cruiser Prado, na kupokelewa kwa mikono miwili na Mkuu wa Shule, Mathew Mutiso, ambaye alimkumbatia kwa furaha. “Ninahisi kama ninaota. Siwezi kuamini niko shuleni—na si shule yoyote bali ya kitaifa. Tulipoenda kununua sare jana nilidhani ninaona ndoto,” alisema Teddy huku akirekebisha tai yake mpya. Aliahidi kuwa na nidhamu na kujituma masomoni. Kwa miaka mingi alikuwa akichora kwenye karatasi zilizookotwa kwa kalamu ya kuazima. “Sasa nina daftari la michoro na seti ya penseli. Niko tayari kuwa msanii niliokuwa nikiota. Nitafanya mamangu ajivunie. Nawashukuru Wakenya wote walionisaidia. Mungu awabariki,” alisema. Mamake, Bi Kadzo, aliketi kimya katika ofisi ya mkuu wa shule, fimbo yake nyeupe ikiwa pembeni—mahali salama zaidi kuliko barabara za vumbi za Malindi. Ingawa hakuweza kuona sare mpya ya mwanawe, aliigusa kwa mikono huku machozi yakimtiririka. Bw Mutiso alisema shule iliamini Teddy anastahili nafasi hiyo kutokana na alama zake 53 na kipaji chake katika mkondo wa Sanaa na Michezo. Bw Fikirini alisema shule ya bweni itampa muda wa kutosha wa kusoma na akahimiza wazazi Pwani kuwapeleka watoto shuleni licha ya changamoto za kiuchumi.