Jeshi la Uganda lakanusha kumteka kiongozi wa upinzani Bobi Wine

Maafisa wa Usalama wa Uganda, Jumamosi walikanusha vikali ripoti zilizodai kuwa mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa rais uliofanyika wiki hii  Robert Kyagulanyi alikuwa amekamatwa, wakitaja taarifa hizo kuwa za “kupotosha na kuchochea fujo.” Polisi waliwahimiza raia kudumisha amani huku taifa hilo likisubiri kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais. Uganda ilifanya uchaguzi mkuu Alhamisi katika mazingira ya taharuki, huku huduma ya intaneti zikiwa zimezimwa kwa siku nne mfululizo, wanajeshi  na maafisa wa usalama walitumwa kote nchini na visa vya ghasia viliripotiwa katika baadhi ya maeneo baada ya wananchi kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge. Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, anawania muhula wa saba madarakani na anaongoza kwa mujibu wa matokeo ya awali kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura. Mpinzani wake mkuu, mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, ana takribani asilimia 20 ya kura. Hata hivyo, Wine ameyapuuza matokeo hayo akiyataja kuwa ya “uongo” na kuwataka wafuasi wake wayapuuze. Akizungumza Jumamosi, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alisema kuwa Wine “hajakamatwa” kama ilivyodaiwa na chama chake cha National Unity Platform (NUP). Alisema kuwa Wine yuko huru kuondoka nyumbani kwake, ingawa kuna hatua za “kuthibiti watu wengine kuingia na kutoka” ili kuzuia matumizi ya makazi hayo kuchochea ghasia. “Haifai kushangaa kuona gari moja au mbili za polisi karibu na makazi ya Kyagulanyi,” alisema Rusoke. Maafisa wa tume ya uchaguzi wanatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya urais Jumamosi, kama inavyotakiwa kikatiba. Mwenyekiti wa tume hiyo alisema Ijumaa kuwa maandalizi yalikuwa yakiendelea vizuri ili kutangaza matokeo kabla ya mwisho wa siku. Uchaguzi huo uligubikwa na changamoto, zikiwemo kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura na hitilafu za mashine za kutambua wapiga kura, hali iliyolazimu maafisa kutumia sajili za karatasi. Rais Museveni alisema alikubaliana na hatua hiyo, lakini Wine alidai udanganyifu mkubwa wa kura na kutekwa kwa maajenti wa chama chake ili kukipa chama tawala faida isiyo halali. Katika taarifa tofauti, chama cha NUP kilidai kuwa jeshi lilimtoa Wine kwa nguvu nyumbani kwake Ijumaa na kumpeleka kusikojulikana. Wine pia alidai kuwa vikosi vya usalama vilizingira makazi yake, hatua aliyoitaja kama kifungo cha nyumbani, na kuwalaumu kwa kuwaua wafuasi wake kadhaa. Kwa mujibu wa NUP, jeshi la Uganda lilimtoa kwa nguvu Wine nyumbani kwake Ijumaa na kumpeleka kusikojulikana. Chama hicho kilisema kupitia mtandao wa X kuwa wanajeshi walimlazimisha Wine kuingia kwenye helikopta na kumpeleka kusikojulikana. Mnamo Ijumaa, Wine alisema vikosi vya usalama vilizingira makazi yake, hali aliyosema ni kifungo cha nyumbani. Pia aliwalaumu wanajeshi kwa kuwaua wafuasi wake 10. “Huu si ujasiri,” aliandika kwenye X. “Wanafanya haya kwa hofu ya wananchi waliowakosea kwa kutenda unyama mwingi. Wanaogopa hasira ya watu baada ya kuiba kura zao.” Siku mbili kabla ya kura, serikali ya Museveni ilikata huduma ya intaneti na simu, hatua iliyotangazwa na shirika la NetBlocks. Tume ya Mawasiliano ya Uganda ilisema hatua hiyo ililenga kudhibiti usambazaji wa taarifa potofu, kuzuia udanganyifu wa uchaguzi na kuchochea ghasia. Hadi sasa, mtandao huo bado haujarejeshwa. Uganda haijawahi kushuhudia mabadiliko ya madaraka ya rais kwa amani tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza zaidi ya miaka 60 iliyopita, huku utawala wa Museveni wa karibu miongo minne ukikosolewa vikali kwa ukandamizaji wa upinzani na matumizi ya nguvu kupindukia.