Tarime. Baadhi ya vijana katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara wameiomba Serikali kuweka mazingira rafiki kwa vijana waliojiajiri, hususan katika sekta zisizo rasmi, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira. Vijana hao wamesema licha ya uhaba wa ajira rasmi, wapo ambao wameamua kutumia fursa zilizopo kujiajiri, lakini wamekuwa wakikumbana na mazingira magumu yanayowakatisha tamaa. Kwa maelezo yao, ugumu huo kwa kiasi kikubwa unasababishwa na baadhi ya mamlaka za Serikali, jambo linalozuia jitihada zao za kujikwamua kiuchumi. Maoni hayo yametolewa leo Januari 17, 2026, wakati wa kikao kati ya vijana wa Tarime na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kilichofanyika mjini Tarime kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za vijana wilayani humo. Wamesema mazingira yasiyo rafiki ya kufanyia kazi yamesababisha vijana wengi kushindwa kutimiza ndoto zao za kujitegemea kiuchumi, hali inayochangia baadhi yao kujihusisha na migogoro isiyo ya lazima na wengine kujiingiza katika vitendo vya uhalifu. Mmoja wa vijana hao, Salvatory Magesa amesema mara nyingi fursa zinazotangazwa hawanufaiki nazo vijana wengi kwa kuwa zinakumbwa na usiri na upendeleo kwa watu wachache. “Kwa mfano, kazi za ufundi zinatangazwa na halmashauri, lakini sisi ambao hatuna ‘connection’ hatupati. Badala yake, wanapewa watu wanaofahamika au wenye uwezo wa kifedha. Sasa sisi ambao hatuna majina wala fedha tutatoboa kweli?” amehoji. Kwa upande wake, Chacha Gibogo amesema vijana wengi wamejiajiri katika sekta ya usafirishaji hususan bodaboda, lakini sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zinazowalazimu baadhi yao kuacha kazi. Naye Haruni Nyagori amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili waendesha bodaboda ni mahusiano yasiyo mazuri kati yao na vyombo vya usalama, hali inayosababisha kukamatwa mara kwa mara, hata kwa makosa yanayohitaji maelekezo tu. “Unaishia kutumia fedha zote kulipa faini badala ya kujikimu. Pia tunafanya kazi katika mazingira hatarishi; barabara ni mbovu. Mfano Barabara ya Rebu imejaa mashimo na ajali hutokea mara kwa mara. Waathirika wakubwa ni sisi bodaboda,” amesema Nyagori. Kwa mujibu wa Nyagori, haki sawa, mazingira rafiki, uwazi na uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kutatua changamoto za vijana, hususan katika suala la ajira. Akizungumza katika kikao hicho, mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni Chifu wa kabila la Wakurya, Christopher Gachuma, amewataka vijana kujipanga vizuri ili waweze kunufaika na fursa zilizopo. Amesema Serikali kwa sasa inahimiza mfumo wa ushirika, hivyo vijana wanapaswa kujiunga katika vyama vya ushirika kulingana na fani zao ili kurahisisha upatikanaji wa fursa. “Yote mliyoyasema yanawezekana kutekelezwa. Mengine hata sisi binafsi tunaweza kusaidia kuyapatia ufumbuzi. Kinachotakiwa ni vijana kujipanga na kuwa na mahusiano mazuri kati yenu, Serikali na watu wazima. Hakuna haja ya migongano isiyo na tija,” amesema Gachuma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka vijana kubadilika kifikra na vitendo ili waweze kutumia kikamilifu fursa zilizopo, akisema wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla vina fursa nyingi za kiuchumi ambazo bado hazijatumika ipasavyo. Ameahidi kushughulikia changamoto zinazotokana na baadhi ya mamlaka za Serikali na kuagiza uongozi wa wilaya ya Tarime kuwatambua vijana wote wenye fani mbalimbali ili waunganishwe na fursa zilizopo. “Nimeshtushwa na madai kuwa mafundi vijana wa Tarime wanakosa kazi wakati kuna miradi mingi ya Serikali inayotekelezwa. Miradi hiyo inapaswa kutekelezwa na mafundi waliopo katika jamii husika. Sasa iweje mafundi wa Tarime wakose kazi?” amehoji. Amesema mara kwa mara anapokagua miradi ya maendeleo huarifiwa kuhusu uhaba wa mafundi, hivyo taarifa za mafundi kukosa kazi zimemshangaza. Aliagiza suala hilo lifanyiwe kazi mara moja na mafundi wa Tarime wahusishwe katika miradi yote bila upendeleo.