Gachagua pabaya kisiasa, wandani wake wanaendelea kumtoroka

KINARA wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, anaonekana kukumbwa na wimbi la kutorokwa na wafuasi wake, hali ambayo wachambuzi wa siasa wanaonya huenda ikapunguza mafanikio aliyopata katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Wanaomtema, wengi wao wakirudi kwa Rais William Ruto, wanasema Bw Gachagua na chama chake cha DCP, wamekuwa wakifanya kazi yao kuwa ngumu kwa kuwaweka katika mgongano wa moja kwa moja na serikali iliyoko madarakani. Kwa upande wake, Bw Gachagua anadai wanaomtoroka ni watu wanaotafuta maslahi yao binafsi na fedha kupitia mkakati wa Rais Ruto wa kuhakikisha anasalia madarakani 2027. Hata hivyo, wakosoaji wake wengi wanamsawiri kama kiongozi asiyevutia kisiasa na asiye na mkakati wa muda mrefu. Kwa mtu aliyeng’olewa mamlakani kama Naibu Rais Oktoba 2024, baada ya kuhudumu kwa miaka miwili pekee, kukataa kufifia kisiasa kumewashangaza wengi, na kumfanya ajipatie nafasi muhimu katika meza ya kuamua mustakabali wa siasa za taifa. Baada ya kufurushwa, Bw Gachagua alianzisha chama cha DCP, akakijenga kuwa chama chenye muundo thabiti na akajitokeza kama mmoja wa watu wanaoweza kuamua mwelekeo wa uchaguzi mkuu wa 2027. Hata hivyo, katika safari hiyo, amekuwa akipoteza wafuasi wake mmoja baada ya mwingine, wa hivi punde akiwa Mbunge wa Juja, Bw George Koimburi. Mbali na Bw Koimburi, wengine waliomtoroka katika ngome yake ya Mlima Kenya ni pamoja na Mbunge wa Maragua Mary wa Maua, Mbunge wa Kangema Peter Kihungi, Mbunge wa Runyenjes Muchangi Karemba, Mbunge wa Githunguri Gathoni wa Muchomba, Mwakilishi wa Wanawake wa Embu Njoki Njeru, miongoni mwa wengine kadhaa. Kwa kuzingatia kasi ya kuondoka kwa washirika wake, mwezi Januari unaonekana kuwa mgumu kwa Bw Gachagua. Taifa Jumapili imebaini kuwa viongozi wawili wakuu wa chama chake tayari wamebadilisha mwelekeo kisiasa, na ni muda tu kabla yao kutangaza rasmi uamuzi wao. Mmoja amepanga mkutano na wanahabari Jumatatu, huku mwenzake akitarajiwa kukutana na Rais Ruto katika Ikulu saa kumi na mbili jioni siku hiyo hiyo. Wawili hao walikuwa na uhasama mkubwa na Rais baada ya vuguvugu la Gen Z, na kurejea kwao kutathibitisha kuwa katika siasa ni maslahi hutawala. Wengi waliomuacha Bw Gachagua wanatoka eneo la Mlima Kenya, jambo ambalo amethibitisha mwenyewe akilaumu “kuingiliwa na serikali,” kauli iliyomlenga moja kwa moja aliyekuwa mkubwa wake, Dkt Ruto. “Ni kweli kwamba ninapoteza baadhi ya wanajeshi wangu wa kisiasa. Lakini hili si jambo la kunitia wasiwasi. Tatizo kubwa kambini mwangu ni upelelezi, kuwindwa na serikali na chama kukua kiasi kwamba baadhi ya wanaowania starehe wanalazimika kushuka kwa kelele,” alisema Bw Gachagua Januari 12, 2026, katika mahojiano na Kameme TV. Hata hivyo, baadhi ya waliomuacha wanasema tatizo si shinikizo la nje pekee, bali pia mienendo ya Bw Gachagua mwenyewe. Bw Koimburi, kwa mfano, anadai kuwa DCP “imegeuka chama cha kidikteta kinachouza tiketi za uchaguzi kwa mnada.” “Gachagua na DCP wanawakilisha ulaghai na hadaa. Chama kilipokea Sh5 milioni kutoka kwa mgombea mwingine ili nitupwe nje Juja. Tiketi za 2027 zinauzwa kwa wanaotoa pesa nyingi zaidi,” alisema Bw Koimburi. Lakini Bw Gachagua alimpuuza mbunge huyo akisema alitaka apendelewe kwa kukabidhiwa tiketi ya moja kwa moja ya uchaguzi mkuu wa 2027, jambo ambalo chama kilikataa. Kupitia taarifa Januari 16 kutoka kwa Katibu Mkuu wa DCP, Bw Hezron Obaga, chama kilisema kutoa tiketi bila mchujo kungeua demokrasia ya ndani ya chama. Seneta wa Nyandarua John Methu anadai Rais Ruto anavuruga DCP na upinzani kwa jumla kwa kuwashawishi viongozi waasi. “Shinikizo, vitisho, kesi na pesa zinatumika kuwavunja wapinzani,” alisema. Hata hivyo, baadhi kama Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga wameonekana kumchangamkia tena Rais Ruto, hatua iliyowapa nguvu wafuasi wa Rais Mlima Kenya. Kauli za kumuunga mkono Rais zimefasiriwa kama pigo kubwa kwa Bw Gachagua. Wengine waliokuwa karibu na Bw Gachagua, akiwemo aliyekuwa msimamizi wake wa mawasiliano Wambugu Ngunjiri, wanasema kiongozi huyo ni “mgumu kufanya naye kazi, dikteta na hutumia hofu kama silaha ya kisiasa.” Kutokana na hali hii, safari ya Bw Gachagua imejaa misukosuko: anasifiwa kwa ujasiri na uthabiti, lakini pia anakosolewa kwa siasa za mgawanyiko na mtindo unaowasababisha washirika wake kumtoroka.