Owalo: Mimi sio mradi wa serikali

ALIYEKUWA Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika ofisi ya Rais William Ruto, Bw Eliud Owalo, amesisitiza kuwa yeye si mradi wa serikali, kufuatia tetesi kuwa uamuzi wake wa kuwania urais mwaka 2027 ni njama ya kudhoofisha Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika eneo la Nyanza. Bw Owalo, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa ICT na Uchumi wa Kidijitali, alisema ameacha kabisa kufanya kazi chini ya wanasiasa binafsi baada ya miaka mingi ya kuwa mwanamikakati wa wagombeaji mbalimbali wa urais katika chaguzi zilizopita. Alianza safari yake ya kisiasa akiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kupitia muungano wa CORD, ambapo alikuwa mkuu wa kampeni za urais mwaka 2013 na msimamizi mkuu wa kampeni. Katika kipindi hicho, alisema alifanya kazi si kwa Raila pekee bali pia kwa vinara wengine wa muungano huo akiwemo Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya. Baadaye alihamia Chama cha ANC ambako alikuwa mshauri wa karibu na mwanamikakati wa Mudavadi, kabla ya kujiunga na Rais Ruto kuanzia mwaka 2019 hadi hivi majuzi alipojiuzulu kufuatia tangazo lake la kuwania urais. Bw Owalo alisema iwapo angekuwa mradi wa serikali, asingejiondoa katika utawala wa Kenya Kwanza. “Kwa nini niondoke serikalini ambako nilikuwa tayari ndani yake, halafu niliendelee kufanya kazi kwa siri? Mimi ni mtu wa maamuzi, asiyeogopa na ninayesema hadharani,” alisema. Alisema alijiuzulu ili awe huru kutekeleza mambo ambayo hangeweza kufanya akiwa serikalini. Hatua yake sasa imebadilisha taswira yake kutoka mshirika wa karibu wa mamlaka hadi mpinzani anayejiandaa kuwania kiti cha juu nchini. Bw Owalo pia alikosoa vikali utawala wa Rais Ruto, akidai umejaa ufisadi na migongano ya maslahi. “Zabuni zinatolewa kwa kampuni za watu wa karibu na maafisa wakuu wa serikali. Katika utawala wangu, nitakuwa na msimamo mkali dhidi ya ufisadi kwa kufanya huduma zote za serikali kuwa za dijitali,” alisema. Hata hivyo, nia yake imezua hisia tofauti. Wachambuzi wengine wanaona ni mkakati wa Rais Ruto kudhoofisha ODM katika ngome zake, huku wengine wakiamini Owalo anatafuta tu kuendelea kuwa na mvuto wa kisiasa. Wengine, hata hivyo, wanamtaka achukuliwe kama chaguo mbadala halisi katika siasa za kitaifa. Bw Owalo mwenyewe anasisitiza kuwa demokrasia ya vyama vingi haiwezi kustawi ikiwa maeneo kama Nyanza yataendelea kutawaliwa na chama kimoja. “Wananchi lazima wapewe fursa ya kuchagua viongozi wao bila shinikizo,” alisema, akiongeza kuwa yuko tayari kushindana na ODM lakini pia kushirikiana nayo kisiasa wakati ufaao.