Oburu aonywa akae rada asinaswe na mtego wa Ruto

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeonywa dhidi ya kukimbilia makubaliano ya kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2027 na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) huku wadau na wachambuzi wakisema ndoa ya kuharakisha inaweza kuisha kwa majuto. Vyama hivyo viwili vikubwa nchini viko mbioni kusuka muungano wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027 ambapo ODM inayoongozwa na Dkt Oburu Oginga inatazamiwa kuunga Rais William Ruto kuwania muhula wa pili. ODM inakumbwa na misukosuko ya ndani, baadhi ya maafisa wake wakuu wakipinga ushirikiano na Rais Ruto ambao Dkt Oburu anachangamkia. Wanaokosoa muungano huo ambao tayari umeanza kusukwa wanahisi kwamba unaharakishwa hata kabla ya chama kutathmini kwa kina chaguo mbadala kutoka kwa washirika wake ndani ya muungano wa Azimio la Umoja. Japo anaonekana kukata kauli kuungana na Dkt Ruto ambaye anatamani zaidi ushirikiano huo kufanikisha azma yake ya kuendelea kuongoza baada ya 2027, Dkt Oburu alisema ODM itazungumza na vyama vingine vilivyo na malengo sawa, lakini akasema chama chake kitapatia kipaumbele mazungumzo na UDA. Vyama hivyo vina ushirikiano chini ya serikali jumuishi. Kulingana na Mbunge wa Suba South, Caroli Omondi, ambaye ametangaza kuwa hatagombea tena kiti chake kwa tiketi ya ODM, chama hicho kinaweza kujikuta katika makubaliano ya haraka yatakayodhoofisha misingi yake ya kisiasa na urithi wa aliyekuwa kiongozi wake, marehemu Raila Odinga. Akizungumza na kituo cha televisheni cha humu nchini Alhamisi, Januari 15, 2026, Omondi alisema ODM inafaa kwanza kujaribu kuwakusanya washirika wake ndani ya Azimio, kama vile Wiper, ili kufanya mazungumzo ya pamoja na Rais William Ruto badala ya kujadiliana peke yake na UDA. “ODM inaweza kuwa na nguvu zaidi ikiketi mezani pamoja na vyama vinavyotaka kushirikiana ndani ya Azimio la Umoja. Kwa njia hiyo, chama kitapata mkataba bora zaidi badala ya kukimbilia makubaliano yasiyochambuliwa kwa kina,” alisema Omondi. Mbunge huyo pia alitoa wito wa uvumilivu wa kisiasa ndani ya ODM, akionya dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wanachama wanaochukuliwa kama waasi au wanaotoa maoni tofauti, hasa kutoka eneo la Nyanza. Alisema demokrasia ya kweli inahitaji kusikilizana na kuheshimiana. Wachambuzi wanahisi kuwa UDA inatumia mgawanyiko unaoshuhudiwa ndani ya ODM kunufaika huku chama hicho cha chungwa kikidhoofika. Bw Omondi anashangaa ni kwa nini uongozi wa sasa wa ODM unapuuza vigogo ambao Raila Odinga alikuwa akiheshimu wakiwemo magavana Profesa Anyang’ Nyong’o (Kisumu) na James Orengo (Siaya), kama viongozi wanaofikiri kwa kina kabla ya kutoa misimamo yao. “Raila alikuwa anamheshimu sana Anyang’ Nyong’o kama mwamuzi tegemeo wa kimkakati. Ukiona watu kama hawa wako kimya, kuna sababu. Sio kila jambo linafaa kujibiwa kwa haraka,” alisema. Hofu ya wachambuzi wa siasa ni kuwa ODM inaweza kuharibu urithi wa Raila Odinga kwa kufanya maamuzi makubwa bila mashauriano mapana. “Raila alijenga urithi mkubwa katika chama hiki. Ni huzuni kuona baadhi ya watu wakikimbilia kuuharibu kwa maamuzi yasiyo na mashauriano ya kina,” asema mchanganuzi wa siasa Dave Opar. Kulingana na Seneta wa Makueni Dan Maanzo, ODM inameza chambo cha UDA ambayo inajijenga baada ya kupoteza nguvu pakubwa katika eneo la Mlima Kenya kufuatia kuibuka kwa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Kwa mujibu wa Maanzo, hali hiyo imelazimisha UDA kutegemea ODM ili kuimarisha nafasi yake kuelekea uchaguzi wa 2027. Maanzo alisema kuwa baada ya Gachagua kuondolewa madarakani na baadaye kujiondoa UDA, ameweza kujijengea ngome imara kupitia DCP, jambo lililopunguza umaarufu wa UDA katika eneo hilo muhimu kisiasa. Alisisitiza kuwa ODM ni chama kikubwa zaidi nchini, chenye mizizi ya kina kote nchini ikiwemo Kaskazini na Kaskazini Mashariki na kwamba chama hicho kinafaa kujadiliana kutoka nafasi ya nguvu na kuepuka makubaliano ya haraka yanayoweza kudhoofisha misingi yake. Kauli hii inaungwa mkono na Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, ambaye ameonya kuwa ODM iko hatarini kujidhoofisha kupitia migawanyiko ya ndani na mbio za kisiasa zisizo na subira. Amisi alisema chama kinafaa kupunguza kasi, kujitathmini na kuheshimu urithi wa Raila Odinga. “Uchaguzi ni 2027, sio Februari 2026. Hakuna haja ya presha ya kisiasa inayochosha chama mapema,” alisema Amisi, akionya kuwa ukosefu wa uvumilivu unaweza kugawanya chama na kukifanya kupoteza mwelekeo. Amisi alionya kuwa ODM inaweza kuishia kama vyama vingine vilivyodhoofika kutokana na migawanyiko ya ndani, akitoa mfano chama cha ANC cha Musalia Mudavadi. Alitoa wito kwa viongozi wakuu wa ODM, akiwemo Oburu Odinga, kupunguza joto la kisiasa na kulinda umoja wa chama.Haya yote yanajiri wakati UDA na ODM zimeidhinisha rasmi kuanza mazungumzo ya kimuundo kuhusu uwezekano wa kuunda muungano kuelekea 2027. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema ODM inapaswa kuchukua tahadhari kubwa ili isije ikaingia kwenye ndoa ya kisiasa itakayodhoofisha misingi yake na kupoteza mwelekeo wa muda mrefu wa chama.