Nyoro afunguka kuhusu bifu yake na Ruto akisisitiza suala la ahadi hewa

HATIMAYE Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, amefunguka kuhusu chanzo cha mgogoro wake mkali na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto. Bw Nyoro anasema mvutano wake na chama kinachoongozwa na Rais William Ruto ulianza pale UDA ilipoacha kutekeleza ahadi ilizowapa Wakenya wakati wa kampeni. Kwa mujibu wa mbunge huyo ambaye awali alionekana kuwa miongoni mwa watu waliokuwa karibu zaidi na uongozi wa UDA, alipata nafasi ya kueleza na kuuza ajenda ya chama hicho kwa wananchi, lakini kile kilichoahidiwa hakikufuatwa baada ya kuingia madarakani. “Ni chama cha UDA kilichokengeuka. Tulipokuwa tukifanya kampeni, na mimi nilipata nafasi ya kuuza ajenda ya chama, nadhani chama kiliacha kile tulichokuwa tumekubaliana kufanya,” alisema Nyoro, akizungumza Jumatano usiku katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga cha humu nchini, Alitaja masuala ya uchumi kuwa eneo kuu ambalo chama tawala kimepokosea Wakenya. Nyoro alisema kuwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, UDA iliwaahidi Wakenya kuwa serikali ingeepuka kukopa kwa kiwango kikubwa, lakini hali imekuwa kinyume na matarajio hayo. “Nimezungumzia masuala kadhaa, lakini jambo kuu ni uchumi. Tuliwaambia Wakenya kwamba hatungekopa pesa nyingi kama tunavyokopa sasa,” alisema. Mbunge huyo pia alishutumu serikali kwa kushindwa kutimiza ahadi katika sekta ya elimu, hasa kuhusu ufadhili wa elimu.Aidha, alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi serikali inavyoshughulikia sauti za wanaotoa maoni tofauti, hususan vijana. “Tuliahidi kupatia elimu kipaumbele kinachostahili, lakini sidhani kama chama kinafanya kile tulichowaambia wananchi, hasa kuhusu suala la ufadhili wa elimu. Pia, nini kimekuwa kikifanyika kwa wale wenye maoni tofauti? Mmeona yaliyowakumba vijana. Tunawekeza sana katika mahusiano ya umma badala ya kuruhusu matokeo yaseme yenyewe,” alisema Nyoro. Bw Nyoro, ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa, alipoteza wadhifa huo kufuatia mvutano wake na chama cha UDA.Nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Alego Usonga, Sam Atandi, kutoka chama cha Orange Democratic Movement (ODM).