Mwanamume taabani kwa madai ya kupokea Sh1.5m ‘akiuza’ barua za kazi ya polisi

MWANAMUME anayedaiwa kupokea kwa njia ya undanganyifu Sh1.5milioni akidai atawasaidia watafuta ajira wanne kujiunga na Idara ya Polisi (NPS) alishtakiwa Ijumaa Januari 16, 2026. Dennis Mugambi Kamwara alishtakiwa katika mahakama ya Milimani kwa kumpora Gichunuku Elius Mutuma Sh1, 540, 000 kati ya Novemba 25 na Desemba 2, 2025. Mahakama ilielezwa na kiongozi wa mashtaka ya umma (DPP) Doreen Njoroge kwamba Kamwara alipokea pesa hizo siku nane baada ya makrutu 10,000 kuteuliwa kujiunga na chuo cha kutoa mafunzo cha polisi-Kiganjo. Zoezi la kuteuliwa kwa makurutu kujiunga na kikosi cha polisi ilikamilishwa November 17, 2025. “Mshtakiwa alimdanganya Bw Mutuma kwamba alikuwa na uwezo wa kuwapeleka jamaa wake wanne kujiunga na kikosi cha polisi,” Bi Njoroge alieleza mahakama. Mshtakiwa alikana shtaka dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana. Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi hilo ila alieleza mahakama Kamwara aliwahi kamatwa Julai 2020 kwa madai sawa na hayo ya kuuza madawa yenye madini ya Omega-3. “Naomba mahakama izingatie kwamba mshtakiwa alitiwa nguvuni Julai 2020 wakati wa maradhi ya Covid pamoja na washukiwa wengine wawili kwa madai ya kutapeli watu katika mtaa wa Zimmerman kwamba anauza madawa ya Omega-3," Bi Njoroge alimweleza hakimu mwandamizi Carolyne Mugo. Hata hivyo mahakama ilielezwa dhamana ni haki ya mshtakiwa ila masuala ya awali hutiliwa maanani uamuzi ukitolewa. Akitoa uamuzi hakimu alisema upande wa mashtaka haujawasilisha ushahidi kwamba mshtakiwa atatoroka ama kuvuruga mashahidi. Hakimu alimwagiza mshtakiwa alipe dhamana ya Sh1 milioni moja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho. Mahakama iliagiza upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala za ushahidi aandae tetezi zake.